Habari

Vigogo kukatiwa maji

Shirika la Maji safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO), limetangaza kuyakatia maji maeneo ya Masaki na Mbezi Beach kuanzia keshokutwa kutokana na kushindwa kulipa deni la zaidi ya Shilingi bilioni moja.

Na Beatrice Bandawe



Shirika la Maji safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO), limetangaza kuyakatia maji maeneo ya Masaki na Mbezi Beach kuanzia keshokutwa kutokana na kushindwa kulipa deni la zaidi ya Shilingi bilioni moja.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Alex Kaaya, alitangaza notisi hiyo ya siku tatu inayoanzia leo kuyakatia maji maeneo hayo sugu, wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari, makao makuu ya DAWASCO, jijini Dar es Salaam.


Akitaja madeni wanayodaiwa katika kila eneo, alisema Masaki ambayo ina wateja 1070 inadaiwa Sh. milioni 574, wakati Mbezi Beach yenye wateja 1271 inadaiwa Sh. milioni 578.
`Natoa notisi ya siku tatu, Jumatatu, Jumanne na Jumatano kwa awamu ya kwanza katika maeneo ya Masaki na Mbezi Beach�Huu ni mwanzo baada ya hapo tunakwenda kwenye maeneo mengine,` alisema.


Bw. Kaaya alisema notisi hiyo inaanza leo na baada ya hapo maeneo hayo watakatiwa maji mpaka watakapolipa madeni yao.


Alitaja maeneo mengine korofi yenye madeni sugu pamoja na deni lao kwenye mabano kuwa ni Ada Estate ( Sh. milioni 527), Mikocheni (Sh. milioni 566), Mwenge (Sh. milioni 463) na Regent Estate (Sh. milioni 200).


Alisema Shirika limeamua kubadili utaratibu kwa kukata kwa maeneo na linaanzia Masaki na Mbezi Beach na baadaye linakwenda kwenye maeneo mengine.


Alisema kushindwa kulipa madeni hayo ni kulisababishia shirika kifo na hataruhusu hali hiyo itokee.


“Tatizo hili linasababisha huduma ya maji kuwa si nzuri na kuweza kusababisha DAWASCO kufa, wakati nia yetu nikutoa huduma endelevu kwa wateja wetu,“alisema Bw. Kaaya.


Alisema Dar es Salaam kuna maeneo yenye nafuu ya maji lakini watu hawataki kuyalipia au wanaolipa ni kwa kiasi kidogo na hali hiyo inaonyesha maji si muhimu kwao.


Akifafanua, Bw. Kaaya alisema kwa upande wa Masaki ni asilimia tano tu ya wateja wanaolipia huduma hiyo na kwa upande wa Mbezi Beach ni asilimia kumi tu.


`Madeni hayo ni ya wakati wa DAWASCO, yale ya nyuma hayahesabiki Tukiendelea namna hii Shirika litakufa,` alisema Bw. Kaaya.


Aliongeza kuwa asilimia 90 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wanakunywa maji bila kulipia.


Kuhusu utaratibu wa kufunga mita za LUKU katika huduma ya maji, Ofisa Mkuu wa Biashara, Bw. Emmanuel Mndolwa, alisema DAWASCO ilifanya majaribo ya kufanya mita hizo katika eneo la Namanga kwa kufunga mita 15 lakini hazikuleta mafanikio.


Alisema kumekuwa na tatizo la watu kutafuta njia mbadala ya kufanya mita hizo zisifanye kazi vizuri ili wasilipe fedha nyingi.


Alisema DAWASCO inawasiliana na Shirila moja la Windhoek, nchini Namibia ambao wanatumia mita za LUKU kwenye huduma ya maji na ambayo imefanikiwa kwa asilimia 100 waweze kuwapa ozoefu.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents