Habari

Vigogo wapandishwa kizimbani kwa kutafuna Mabilioni

Vigogo 6 wanaotuhumiwa kuhusika ufisadi wa soko la Kimataifa la Mwanjelwa lililopojijini Mbeya wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mbeya na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi.

Waliopandishwa kizimbani Mahakamani hapo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji hilo, Elizabeth Munuo (65), aliyekuwa Meya wa jiji hilo, Athanas Kapunga (70) na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo Dk. Samwel Lazaro ambaye kwa sasa ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe,Mtunza Hazina wa Jiji hilo, James Jorojik (62), aliyekuwa Mwasibu wa jiji hilo, Tumaini Msigwa (47) na Mhandisi wa jiji hilo, Emily Maganga (42).

Mwendesha mashtaka wa serikali, Shadrack Martin, akisaidiwa na Hebel Kihaka pamoja na Baraka Mgaya wakati akiwasomea mashtaka yanayowakabili vigogo hao alisema wote kwa pamoja walitenda makosa ya uhujumi uchumi kati ya mwaka 2008 na 2013 hivyo kuisababishia serikali hasara kubwa.

Katika Shtaka la kwanza mwendesha mashtaka huyo alisema linawahusu watuhumiwa wawili ambao ni Athanas Kapunga ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Mbeya na Elizabeth Munuo ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji ambao wanadaiwa kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya Shilingi Bilioni 3.3, ambapo wanadaiwa kusaini mkopo wa kiasi hicho cha fedha kutoka katika Benki ya CRDB ambao ulianza kulipiwa riba kabla ya kuanza kujengwa kwa Soko hilo la Mwanjelwa kinyume cha vifungu vya sheria namba 57 (1) na 60 (1) na (2) vya Sheria za uhujumu uchumi Sura ya 200 ya mwaka 2002.

Martini alisema shtaka la pili linawahusu Dk.Samwel Lazaro, James Jorojik, tumain Msigwa na Emily Maganga ambao kwa pamoja wanadaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuidhinisha malipo ya shilingi milioni 304,470,500 kwa Mkandarasi aliyekuwa anajenga soko hilo, Nandhra Engineering and Constaction ltd wakati kazi hiyo ilikuwa tayari imefanywa na Kampuni ya Tanzania Building Works ltd.

Aidha Washtakiwa wa Shataka namba mbili pia wanashtakiwa kwa kosa la tatu la kuisababishia Halmashauri ya Jiji hasara ya shilingi 1,140,228,750 kwa kuidhinisha malipo ya fedha hizo kwa wakandarasi Tanzania Building Works na Nadhra Engineering kwa ajili ya ujenzi wa Soko hilo wakati kazi iliyotajwa haikuwemo kwenye Mkataba.

Washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa wakitetewa na Mawakili watatu wakiongozwa na James Kyando, Baraka Mbwilo na Secilia Luhanga ambao waliiomba Mahakama hiyo kutoa maelezo kuhusu uwezekano wa wateja wao kupata dhamana.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mbeya, Michael Mteite alisema Mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi hivyo washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu hadi Agosti 29, Mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents