Habari

Viongozi CUF wanusurika kuuawa na majambazi

VIONGOZI kadhaa wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiwemo wabunge wanne, usiku wa kuamkia jana, wamenusurika kuuawa na majambazi katika pori la Muhoro, wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

na Kulwa Karedia

 

VIONGOZI kadhaa wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiwemo wabunge wanne, usiku wa kuamkia jana, wamenusurika kuuawa na majambazi katika pori la Muhoro, wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

 

Wabunge walionusurika wametambuliwa kuwa ni Mkiwa Kimwanga (Viti Maalum), Severina Mwijage (Viti Maalum), Mwadini Abbas Jecha (Wete – Pemba) na Shoka Hamis Juma wa Jimbo la Micheweni.

 

Wabunge hao walikuwa wakisafiri kutoka wilayani Tunduru, ambako walikwenda kushiriki kampeni za uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita. Walikuwa wakirejea Dar es Salaam kwa njia ya barabara.

 

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Vijana Taifa wa chama hicho, Said Abdallah Miraji, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 3.10 za usiku.

 

Alisema walipokuwa wakisafiri katika pori hilo, kundi la watu waliokuwa na silaha nzito kama Sub Machine Gun (SMG), walilivamia gari walilokuwamo wabunge hao na kuanza kufyatua risasi.

 

“Tuliamini kuwa wote tutakufa pale baada ya majambazi yale kuanza kupiga risasi ovyo na kutuamuru kukaa kimya bila kupiga kelele kwa vile walikuwa na kazi ya kutupora mali zetu,” alisema Miraji ambaye naye alikuwa mmoja wa watu waliokumbwa na mkasa huo.Alisema, Mbunge wa Wete, alijeruhiwa vibaya baada ya risasi moja kupenya kwenye mabati ya gari na kumpata sehemu za usoni kwenye jicho lake la kulia.

 

“Hali ya mbunge huyu si nzuri sana na tumemkimbiza Hospital ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kwa vile jicho lake kwa sasa limezibwa kwa bandeji, hatujui kilichomo ndani,” alisema Miraji.

 

Miraji alisema mbali ya wabunge hao kunusurika katika tukio hilo, watu wawili wanasadikiwa kuuawa kutokana na tukio hilo kwa vile yeye mwenye aliwashuhudia.
Alisema gari lililokuwa likitumiwa na wabunge, lenye namba za usajili T 736 ANP aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya chama hicho, limeharibiwa vibaya kutokana na risasi zilizopigwa na majambazi hayo.

 

Alisema katika tukio hilo, wabunge hao waliporwa zaidi ya sh milioni 1.3 taslimu, simu sita za mkononi zenye thamani ya zaidi ya sh milioni mbili, mabegi ya nguo, mikufu na hereni za dhahabu walizokuwa wamevaa.

 

Alisema miongoni mwa majambazi hayo, mmoja alikuwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zilizoonyesha kuwa namba yake ya uaskari ni D 2121.

 

Aliyataja baadhi ya magari ambayo yaliwekwa chini ya ulinzi na majambazi hayo kuwa T 416 AAA aina ya Isuzu, T 705 AHP, T 945 ADV aina ya Scania na T 280 ABV aina ya Fuso.

 

Alisema suala hilo halina uhusiano wowote wa kisiasa na wala chama chake hakiamini kama kimehujumiwa juu ya tukio hilo.

 

Mkurugenzi huyo ameliomba Jeshi la Polisi nchini kuongeza nguvu za ulinzi katika eneo hilo kwani watu wanaoonekana kufanya vitendo hivyo ni wakazi wa eneo hilo, wakisakwa wanaweza kutiwa mbaroni.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents