Moto Hauzimwi
TECNO Spark 2

Viongozi vyuo vikuu watakiwa kukutana na wanafunzi

VIONGOZI wa Vyuo Vikuu nchini wametakiwa kutambua wajibu wao wa kukutana mara kwa mara na wanafunzi wao pindi migogoro na matatizo yanapojitokeza kabla ya kuleta madhara makubwa kwa Vyuo husika na Serikali, imeelezwa.

John Nditi, Morogoro


VIONGOZI wa Vyuo Vikuu nchini wametakiwa kutambua wajibu wao wa kukutana mara kwa mara na wanafunzi wao pindi migogoro na matatizo yanapojitokeza kabla ya kuleta madhara makubwa kwa Vyuo husika na Serikali, imeelezwa.


Rai hiyo imetolewa na aliyekuwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Moses Warioba, katika hotuba yake wakati wa sherehe ya kuthamini mchango wake tangu kilipokuwa Chuo cha Maendeleo Mzumbe (IDM) kwa kipindi cha miaka mitano tangu chuo hicho kilipopandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu kamili.


Profesa Warioba (57), kutokana na kanuni ya mkataba kuwa Makamu Mkuu wa Chuo wa vyuo Kikuu kwa vipindi viwili kwa miaka mitano, hakuweza kuongezewa kipindi kingine kutokana na umri wake wa kustaafu kubakia miaka mitatu.


Amepewa majukumu mengine kwa kushirikiana na chuo hicho kufanya utafiti wa kazi mbalimbali za maendeleo ya Chuo. Hivyo alisema kutokana na uzoefu wake katika uongozi wa chuo hicho, wakati umefika kwa viongozi wanaosimamia Vyuo Vikuu nchini kuanza kujenga utamaduni wa kuwa karibu na wanafunzi katika suala zima la utatuzi wa migogoro na kuzuia migomo.


Alisema kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano cha kuongoza Chuo hicho hapakuweza kujitokeza migomo ya wazi kutokana na ushirikishaji wa karibu wa kusikiliza matatizo ya wanafunzi na mahitaji yao ya msingi.


“Sio kwamba hapakuwa na migomo…ilikuwepo lakini tulikuwa tuwawahi kuwasikiliza wanafunzi nini mahitaji yao ya msingi na tunamalizana nao kabla ya kutoka nje,” alisema Profesa Warioba na kuongeza; “ Tulikuwa na utaratibu wa kukutana na wanafunzi kuzungumza nao na kuwachukulia uzito mkubwa na kuyashughulikia na hatimaye tunaelewana …utakuta ni tatizo la kuchelewachelewa kwa fedha, posho na kuilalamikia Serikali… hivyo sisi tunachukua jukumu na kupeleka Serikalini,” alisema Profesa Warioba.


Hivyo kutokana na hali hiyo amewashauri viongozi hao kutosubiri migogoro ya wanafunzi kuwa mikubwa hadi kufikia migomo kwa kuwa hali hiyo inaleta sifa mbaya kwa viongozi wa vyuo na upande mwingine katika Serikali. “Sasa ni wakati wa kujenga utamaduni wa viongozi wetu wa vyuo vikuu inaposikika dalili za migogoro ni kuchukua hatua za kuingia kufanya majadiliano yenye kufikiwa maamuzi mazuri bila kuathiri uchumi wa nchi, kwa vile migomo inaleta hasara kubwa kwa pande zote,” alisema Profesa Warioba.


Awali, Makamu wa Mkuu mpya wa chuo hicho, Profesa Joseph Kuzilwa, alisema kuwa katika kipindi cha Uongozo wa Profesa Warioba, Chuo hicho kimeweza kupata mafanikio makubwa ya kuongeza idadi ya wanafunzi wake kutoka 1,100 mwaka 2002 hadi kufikia 3,500 mwaka huu.


Source: Habari Leo

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW