Habari

‘Vipodozi huotesha ndevu wanawake’

SERIKALI imesema ni muhimu kwa wananchi kutambua kuwa weupe hauna maana ya uzuri, na kuonya kuwa baadhi ya vipodozi husababisha wanawake kuota ndevu.

Na Jacqueline Liana, Dodoma


SERIKALI imesema ni muhimu kwa wananchi kutambua kuwa weupe hauna maana ya uzuri, na kuonya kuwa baadhi ya vipodozi husababisha wanawake kuota ndevu.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda, alisema hayo bungeni jana, alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mohamed Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF).


Mnyaa alitaka kujua uhusiano wa vipodozi na hali iliyopo ya wanawake wengi wanaovitumia kuota ndevu. Dk. Aisha alisema baadhi ya vipodozi vina homoni za kiume, na mwanamke akivitumia humsababishia kuota Ndevu; akionya kwamba, wanawake wanapaswa kufahamu kuwa mweupe hauna maana ya uzuri.


Katika swali la msingi, Parmukh Singh Hoogan (Kikwajuni-CCM) aliuliza kwamba, kuna baadhi ya wananchi wanapendelea kutumia dawa za kuchubua ngozi na inasemekana zinasababisha madhara kwa afya ya watumiaji.


Hoogan alitaka kujua ni madhara ya aina gani, na kama serikali inafahamu dawa hizo zimesambaa kwenye masoko licha ya kuwa zimepigwa marufuku.
Dk. Aisha alisema matumizi ya dawa za kuchubua ngozi, hususan zile zenye viambato vya sumu husababisha madhara kwa watumiaji.


Alitaja baadhi ya madhara hayo kuwa ngozi kuwa na mabaka meusi na meupe pamoja na kukunjamana; kuwa nyembamba sana, laini na endapo itapata jereha haiponi haraka. Mengine ni kutokwa na chunusi kubwa, kupata mzio wa ngozi, muwasho na athari endapo itapata mwanga wa jua; madhara katika ubongo, figo, maini na mapafu.


Alisema watumiaji pia huweza kupoteza fahamu mara kwa mara na kusababisha saratani ya damu, ngozi, maini, ubongo na mapafu.
Naibu Waziri alisema mjamzito anayetumia vipodozi hivyo kwa muda mrefu huweza kusababisha mtoto aliye tumboni kuathirika, na upo uwezekano wa kuzaliwa akiwa na mtindio wa ubongo.


Alisema serikali inafahamu dawa hizo zimesambaa kwenye masoko, licha ya kupigwa marufuku, kwani baadhi ya wafanyabiashara wa vipodozi wamekuwa wakiviingiza kwa kificho. Dk. Aisha alisema zipo aina 933 za vipozi ambavyo vimethibitishwa kuwa na ubora na usalama kwa afya ya
watumiaji na vinaruhusiwa kuuzwa nchini.


Alisema hatua ambazo serikali imechukua kupambana na matumizi ya vipodozi hivyo ni upigaji marufuku wa matumizi ya aina 182 ya vipodozi vilivyothibitika kuwa na sumu. Serikali pia hufanya ukaguzi katika vituo vya mpakani na maduka ya vipodozi kwa kushirikiana na wasimamizi wa sheria kutoka taasisi nyingine za umma kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).



Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents