Habari

Vituo vingi vya petroli wezi

Taasisi ya Wakala wa Vipimo nchini imebaini kuwa asilimia 77 ya pampu zote za kujaza mafuta mjini Dodoma zinapunja wateja.

Na Mwandishi Wa Nipashe



Taasisi ya Wakala wa Vipimo nchini imebaini kuwa asilimia 77 ya pampu zote za kujaza mafuta mjini Dodoma zinapunja wateja.


Taarifa iliyotolewa na Wakala kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa hali hiyo imebainika baada ya kufanya msako wa ghafla katika vituo vya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.


Ukaguzi huo ulifanywa na Wakala wa Vipimo, kuanzia Julai 23 hadi jana. Zoezi hilo lililoongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo, Bw. Ali Tukai, pia lilihusisha wakaguzi wa vipimo wa Ofisi ya Vipimo Dodoma na Makao Makuu Dar es Salaam.


Katika msako huo ilibainika kuwa, katika kipimo cha ujazo wa lita 20, pampu hizo zilikuwa zinapunja kwa kati ya mililita 100 hadi mililita 760. Vituo vilivyokuwa na pampu zinazopunja kwa kiasi kikubwa ni OIL COM (Kizota), na TIOT (Makole).


Aidha, ukaguzi huo wa kushtukiza ulibaini kituo kimoja ambacho “seal“ za pampu zake zote nne zilikuwa zimevunjwa na pampu hizo kupunja. Mmiliki wa kituo hicho alitozwa faini kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Na. 20 ya mwaka 1982.


Pampu hizo zilifungwa hadi zilipofanyiwa marekebisho na kuhakikiwa upya na maafisa vipimo.


Kazi ya kurekebisha pampu hizo ilifanywa ili kuepusha athari ya mji mzima wa Dodoma kukosa huduma ya mafuta wakiwemo Waheshimiwa Wabunge ambao wanaendelea na majadiliano ya hotuba za bajeti za wizara mbalimbali mjini Dodoma.


Mji wa Dodoma una jumla ya pampu 84 ambazo zote zilikaguliwa katika zoezi hilo.


Pampu 18 zilibainika kuwa mbovu wakati 51 zilibainika kupunja wateja.


Taasisi ya Wakala wa Vipimo imetoa rai kwa wananchi ya kuwafichua wamiliki wa vituo ambavyo pampu zake zinawapunja mafuta.


Taarifa hizo zitolewe kwa ofisi za vipimo zilizoko katika mikoa yote nchini au katika ofisi zake za Makao Makuu zilizopo katika jengo la Mwalimu, Ilala – Dar es salaam.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents