Waachana na muafaka waubiri uchaguzi 2010

CUFChama cha Wananchi (CUF) kimejibu kauli iliyotolewa na Rais Aman Abeid Karume wa Zanzibar ya kuwapa sharti viongozi wa chama hicho kabla ya kukutana kwenye mazungumzo ya kuleta muafaka wa kisiasa visiwani humo

Chama cha Wananchi (CUF) kimejibu kauli iliyotolewa na Rais Aman Abeid Karume wa Zanzibar ya kuwapa sharti viongozi wa chama hicho kabla ya kukutana kwenye mazungumzo ya kuleta muafaka wa kisiasa visiwani humo.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Zanzibar juzi, Rais Karume alimtaka Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kumtambua kwa heshima kuwa ni rais halali wa Zanzibar aliyechaguliwa kwa kura nyingi, kabla ya kukutana naye.

 

Majibu ambayo CUF imesema sasa imeamua kuachana na yote na kusubiri uchaguzi mkuu mwaka 2010 na kubainisha kwamba ‘kikiporwa’ ushindi kwenye uchaguzi huo Zanzibar haitatawaliwa wala kutawalika.

 

Aidha Chama hicho kimemsikitia sana ais Karume kwa kudai kuwa amepoteza nafasi muhimu kwa kuweka sharti gumu la kukutana viongozi wa chama hicho hivyo wameamua kuacha mambo hayo kama yalivyo.

 

Akizungumza na mwandishi kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma, Bw. Salim Biman, alisema “tunasubiri Rais Karume amalize muda wake wa uongozi uliobakia ili ahukumiwe na historia”
“Naweka wazi kwamba mimi sina tatizo na Maalim Seif kukutana naye na kuzungumzia mustakabali wa kisiasa Zanzibar, lakini anitambue kwanza kuwa ni Rais wa niliyechaguliwa kwa kura nyingi kuongoza visiwa hivi,” alisema Rais Karume wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu juzi.

 

Kauli hiyo ya CUF imekuja siku moja baada ya Rais Karume kuweka msimamo wake wazi kwamba atakuwa tayari kukutana na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharrif Hamad, mara baada ya chama hicho kumtambua.

 

Hata hivyo msimamo huo wa Rais Karume umeonesha kuwakatisha tamaa wana-CUF. “Tumempa nafasi muhimu sana ameipoteza hivyo inabidi afahamu kuwa amebakiza miaka miwili ili akae pembeni, akiwa nje ya madaraka historia itamhukumu,” alisema Bw. Biman.
Aliongeza kusema “Tunaelekeza nguvu zetu zote mwaka 2010 katika uchaguzi mkuu kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kweli.Uchaguzi wa 2010 hataibiwa kura mtu vinginevyo Zanzibar haitatawalika,” alisema Bw. Biman na kuongeza kuwa mwaka 1995, 2000 na 2005 chama hicho kiliibiwa kura lakini sasa hali hiyo haitakubalika tena.

 

Katika uchaguzi wa mwaka 2010 ngoma itakavyopigwa ndivyo itakavyochezwa. “Mchezo ukichezewa gizani ndiko tutakapochezea, kama ni kwenye tope huko huko na kama ni kwenye uwanja huru tutawafuata huko huko,”alisema

 

Alisema kauli ya Rais Karume ya kuwataka wana CUF wamtambue ndipo afungue milango ya mazungumza na baada ya kumaliza awape chai wanywe na kisha kuondoka ni ya kudhalilisha Wazanzibar.

 

“Tulitegemea atatumia busara lakini yeye ameenda mbali kwenye ushabiki wa kisiasa kwani kauli ya kusema tumtambue kwanza haina mantiki,” alisema Bw. Biman.

 

Alisema kauli ya Rais Karume kuwa hawezi kuchagua Wapemba kwenye Baraza lake wa Mawaziri kwa sababu walimnyima kura ni kinyume na matakwa ya Katiba kwani inaendeleza vitendo vya ubaguzi.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents