Habari

Waajiri waagizwa kuwasilisha makato ya fidia kwa wakati

SERIKALI imewaagiza Waajiri wote nchini kuwasilisha kwa wakati michango ya mafao ya fidia kwa wafanyakazi ili kuwawezesha watumishi wao kupata huduma za matibabu pindi watakapoumia au kuugua wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mh. Jenista Mhagama akiongea na wadau mbalimbali (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijini Dar es Salaam

Agizo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Ulemavu) Jenister Mhagama wakati alipokuwa akizindua huduma za utoaji wa mafao ya fidia na ubia baina ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) na watoa huduma za afya nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mh. Jenista Mhagama Mh. Jenista Mhagama akizindua Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Kushoto ni Naibu Waziri Mh. uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam

Mhagama alisema suala la uchangiaji wa mafao hayo sio la hiari ila lipo kisheria na hivyo ni wajibu wa waajiri wote nchini kuhakikisha kuwa wafanyakazi wao wanaingizwa katika mfumo huo ili kuwawezesha wafanyakazi kuwa na uhakika wa kulipwa fidia pindi wanapokuwa kazini.

“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali imelipa michango yote ya wafanyakazi wake, na huu ni mfano unaopaswa kuigwa na waajiri wengine nchini, na natoa rai kwa Chama cha Waajiri Nchini (ATE) na Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA) linasimamia suala hili” alisema Mhagama.

Mkurugenzi Mtendaji Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Masha Mshomba akiongea na wadau mbalimbali kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijini Dar es Salaam

Aidha Mhagama alisema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa wafanyakazi nchini ni kusaidia kutatua kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi, ambao wamekuwa wakilalamikia huduma hafifu zinazotolewa pindi wapatapo majanga mbalimbali wakiwa kazini ikiwemo ajali na vifo.

Waziri Mhagama alitaka Bodi ya mfuko huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria zilizopo ili kuhakikisha kuwa waajiri wote hususani wa sekta binafsi wanawasilisha michango kwa wakati.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Emanuel Humba akiongea na wadau mbalimbali kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijini Dar es Salaam

Akifafanua zaidi Waziri Mhagama aliuataka mfuko huo kujitangaza zaidi kwa sekta zisizo rasmi ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hususani wa kipato cha chini kujiunga na mfuko huo na kuwasaidia kufaidi huduma zinazotolewa.
“Natoa rai kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini ikiwemo wa WCF mjitangaze katika sekta zisizo rasmi ikiwemo waendesha bodaboda, akina mama lishe, kwa kuwa idadi yao ni kubwa na hiyo itawezesha kupata wanachama wengi zaidi” alisema Mhagama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Musomba alisema hadi kufikia sasa mfuko huo umeweza kutoa usajili wa waajiri 5945 pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watumishi wa mfuko huo ikiwemo madaktari.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mh. Antony Mavunde akiongea na wadau mbalimbali (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijini Dar es Salaam

Aidha Musomba anasema pia mfuko huo umeingia ubia na taasisi 7 za utoaji huduma za afya nchini, ambazo ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.

Musomba anazitaja taasisi nyingine kuwa ni Strategis, AAR, mfuko wa Jubilee, na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo taasisi hizo zinazoendelea kushughulikia kesi 189 zilizolipotiwa katika mfuko huo. Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Aggrey Mwinuka alisema mfumo huo wa fidia umekuja katika wakati muafaka kwa kuwa sheria zilikuwepo katika vitabu na hazikuwa na utekelezaji uliokusudiwa.

Mwinuka alisema ili kuhakikisha kuwa malengo ya mfuko huo yanatekezeka ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa inafanya majadiliano ya mara kwa mara na waajiri ili kuangalia viwango vya makato ya michango ya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi.

Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Emmanuel Homba alisema uwekaji wa mfumo wa mafao ya fidia utawezesha wafanyakazi katika sekta za umma na binafsi kuchangia kikamilifu katika Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

Na Ismail Ngayonga; Picha na Benjamin Sawe-Maelezo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents