Habari

Wabunge CCM waapa kufa au kupona na Mkataba wa Richmond

BAADHI ya wabunge wa Bunge la Muungano, wameeleza kusikitishwa na hatua ya serikali ya kulitolea maelezo suala la mkataba kati ya Richmond na Shirika la Umeme (TANESCO) kwenye vyombo vya habari badala ya bungeni.

na Martin Malera, Dodoma


BAADHI ya wabunge wa Bunge la Muungano, wameeleza kusikitishwa na hatua ya serikali ya kulitolea maelezo suala la mkataba kati ya Richmond na Shirika la Umeme (TANESCO) kwenye vyombo vya habari badala ya bungeni.



Wameapa kulifuatilia suala hilo, ambalo linategemewa kujadiliwa wiki hii katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini hapa, hadi waliohusika katika mkataba huo wawajibishwe.



Msimamo huo wa wabunge, umetokana na hatua ya gazeti moja la Kiswahili litolewalo kila wiki, kuchapisha barua inayodaiwa kuandikwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini, wakati huo, Ibrahim Msabaha, akimtahadharisha kuwa makini kuhusu mkataba na Kampuni ya Umeme ya Richmond Development Corporation. Dk. Msabaha sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.



Habari za kuaminika zinasema kuwa, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakutana leo mjini hapa na Waziri Mkuu, kuhusu suala la Richmond, huku wakiwa na siri kubwa moyoni ya kufichua ukweli wa suala hilo linaloisumbua serikali kwa muda mrefu.



“Labda chama kinataka kutuziba mdomo kuhusu suala hili, lakini hakitafanikiwa, kwani wabunge tumeapa kufa au kupona kulifuatilia suala hili mpaka ukweli ujulikane,” kilisema chanzo chetu cha habari.



Mbali ya wabunge wa CCM, wabunge wa kambi ya upinzani, nao wameandaa hoja binafsi kuhusu suala la mkataba wa Richmond uliotumia zaidi ya sh bilioni 200, lakini bado kampuni hiyo imeshindwa kuzalisha umeme na kuamua kutoa zabuni hiyo kwa kampuni dada ya Dawons.



Vyanzo vya habari viliiambia Tanzania Daima jana kuwa, juzi na jana, baadhi ya wabunge wa CCM walikuwa na vikao visivyo rasmi kwa nyakati tofauti kujadili uhalali wa serikali kutolea ufafanuzi suala la Richmond kupitia vyombo vya habari badala ya kulileta katika vikao na kamati za Bunge.



Katika barua hiyo ambayo inadaiwa iliandikwa Septemba 21, mwaka jana, Lowassa anajaribu kujivua lawama kuwa hahusiki na matatizo yaliyojitokeza katika mkataba wa Richmond kwa madai kuwa ni Waziri Msabaha ndiye alikuwa akiushughulikia.



Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kichwa cha habari ‘Yah: Kampuni ya Richmond Development Company’, Waziri Mkuu pamoja na mambo mengine alisema: “Kama unavyofahamu, yapo maneno mengi sana yanayosemwa kuhusu uwezo wa kampuni tajwa kuagiza Gas Turbines kama ilivyopewa mkataba na Tanesco baada ya kushinda zabuni.



“Inawezekana hivi vikawa ni vita vya kibiashara, lakini kwa sababu maneno haya yanasemwa na watu wengi na tofauti, ni vizuri UKAJIRIDHISHA kwamba kampuni hii itaweza kutekeleza kazi hiyo,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.



Wabunge hao pia wanahoji uhalali wa serikali kumtwisha Dk. Msabaha mzigo wa Richmond huku ikijua kuwa waziri huyo pamoja na wengine wote, hawana uwezo wa kuingia na kuidhinisha mikataba ya mabilioni ya fedha bila suala hilo kufikishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kwenye Baraza la Mawaziri.



Mmoja wa wabunge ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, alisema kuwa serikali imedhamiria kumfanya Dk. Msabaha kuwa ‘mbuzi wa kafara’ katika suala la Richmond, lakini wamejiandaa kumtetea kwa hoja, kwani waziri huyo hana mamlaka ya kuidhinisha mkataba huo wa mabilioni ya fedha.



Baadhi ya mambo yanayohojiwa na wabunge wa CCM, ambayo wameahidi kuwa, lazima kesho yatalipuka kwenye kikao hicho, ni pamoja na nani mmiliki wa Kampuni ya Richmond na kwa nini serikali imeshindwa kurejesha fedha hizo zaidi ya sh bilioni 200 baada ya kampuni hiyo kushindwa kuzalisha umeme.



Wabunge hao wanasema fedha zilizotumika kuingia mkataba na Richmond pamoja na zile zinazotumika kwenye kampuni zingine za kukodi kuzalisha umeme, zingeweza kujenga mabwawa zaidi ya matano ya kuzalisha umeme kama bwawa la Mtera.



Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1977 na kumalizika 1981 kwa gharama ya sh milioni 318.56 na ujenzi wa kituo cha umeme wa megawati 80, ilikuwa sh milioni 15.86.



“Fedha za mkataba wa Richmond kama zingetumika kujenga mabwawa kama ya Mtera, tungekuwa na mabwawa zaidi ya matano na suala la umeme lingebaki kuwa historia,” alisema mbunge huyo.



Wakati akijadili muswada wa rushwa wiki iliyopita, Mbunge wa Kyela, Dk. Harison Mwakyembe alielezea kushangazwa kwake na hatua ya serikali kupeleka barua ya siri ya waziri mkuu kwa gazeti hilo wakati Bunge na hata kamati za Bunge hazina taarifa ya kuwapo kwa barua hiyo.



“Sisi wabunge na kamati husika, hatujaonyeshwa mkataba wa Richmond, japo tumejitahidi kuomba, lakini hatujapewa maelezo yoyote kuhusu sakata la Richmond. Kwa nini serikali haioni umuhimu wa kulileta suala hili bungeni na kuamua kuthamini vyombo vya habari?” alihoji Dk. Mwakyembe katika mchango wake huo.



Hadi sasa, Tanzania ina miradi ya dharura mitano ya kuzalisha umeme wa kukodi. Mbali ya Richmond ambayo sasa ni Dowans, pia kuna mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 40 kutoka Kampuni ya Aggreko ya Falme za Kiarabu (UAE) ambao unagharimu dola za Kimarekani milioni 61, umeme wa megawati 100 kutoka Kampuni ya WARTSILA ya Finland ambao unagharimu Euro 57,550,000 na umefungwa Ubungo.



WARTSILA pia inatarajia kujenga mtambo mwingine wa kuzalisha umeme wa kukodi eneo la Tegeta, Dar es Salaam na unatarajiwa kugharimu Euro milioni 41 na mradi mwingine wa megawati 40 uko mjini Mwanza ambao unaendeshwa na Kampuni ya Alstom, unaogharimu dola za Kimarekani milioni 116.



Richmond iliingia mkataba na TANESCO wa kuzalisha umeme wa megawati 100 katika kipindi ambacho nchi ilikuwa inakabiliwa na tatizo kubwa la umeme kuliko wakati mwingine wowote.



Hata hivyo, Richmond hawakuweza kutimiza masharti na badala yake shughuli za kampuni hiyo zilichukuliwa na Kampuni ya Dowans ambayo ilitakiwa kuanza kuzalisha umeme hadi Machi mosi mwaka huu, lakini haijaweza kufanya hivyo.



Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents