Habari

Wabunge kumbana Meghji leo

Mjadala mzito kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha (2007/08), unatarajiwa kutawala Bungeni wakati leo Wabunge watakapoanza kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji.

Na Boniface Luhanga, Dodoma



Mjadala mzito kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha (2007/08), unatarajiwa kutawala Bungeni wakati leo Wabunge watakapoanza kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji.


Waziri Meghji, aliwasilisha Bungeni hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha Alhamisi iliyopita.


Kwa mujibu wa ratiba ya Ofisi ya Bunge, Wabunge leo wataanza kuchangia hotua hiyo baada ya kipindi cha maswali na majibu hadi Ijumaa ijayo.


Hata hivyo, mjadala wa hotuba hiyo, unatarajiwa kuwa mkali kutokana na bajeti hiyo kuanza kulalamikiwa na wadau wengi muda mfupi baada ya Waziri Meghji kuiwasilisha Bungeni kwa madai kwamba, hailengi kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini.


Kwa hali ilivyo, Wabunge wengi wanatarajiwa kuibana serikali ili iweze kuondoa ushuru kwenye mafuta ya petroli na dizeli.


Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, kupanda kwa bei ya petroli na dizeli, kutasababisha kupanda bei kwa bidhaa nyingi.


Kambi ya upinzani ambayo leo Waziri wake Kivuli wa Fedha, atawasilisha hotuba ya kuichambua hotuba ya Waziri wa Fedha, tayari ilionyesha kutoridhishwa na Bajeti hiyo ya Serikali.


Baadhi ya Wabunge wa Upinzani ambao tayari wametoa dukuduku lao kuhusiana na Bajeti hiyo, ni Bw. John Cheyo (UDP-Bariadi Mashariki), Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA-Karatu) na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Bw. Hamad Rashid (CUF).


Viongozi hao wa upinzani kwa nyakati tofauti, walikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari muda mfupi baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha Bungeni hotuba yake, wakisema Bajeti hiyo haitamsaidia mwananchi wa kawaida.


Wabunge hao walisema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, kitendo cha serikali kupandisha ushuru wa mafuta ya petroli na dizeli, kwa vyovyote vile kitasababisha nauli za mabasi kupanda sambamba na bidhaa mbalimbali muhimu.


Hata hivyo, kwa upande wake, Serikali imeelezea kuwa, hatua hiyo ni muhimu kwani ndiyo njia pekee na ya uhakika ya kukusanya mapato yake kwa shughuli mbalimbali za maendeleo hususan ujenzi na ukarabati wa barabara.



Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents