Habari

Wabunge wahoji mkatabawa TICTS

BAADHI ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamehoji kitendo cha serikali kuongeza muda wa mkataba wa kampuni ya upakuaji mizigo bandarini ya TICTS, ilhali muda wa awali ukiwa haujamalizika.

na Tamali Vullu

 

BAADHI ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamehoji kitendo cha serikali kuongeza muda wa mkataba wa kampuni ya upakuaji mizigo bandarini ya TICTS, ilhali muda wa awali ukiwa haujamalizika.

 

Wabunge hao ambao ni wajumbe wa Kamati ya Miundombinu, pia wamehoji ukimya wa serikali baada ya uongezaji wa muda katika mkataba kutoka miaka 10 hadi 25.

 

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Anne Kilango Malecela (Same Mashariki-CCM), alisema jana kuwa awali, mkataba huo ulikuwa wa miaka mitano, lakini hata kabla muda huo haujamalizika, serikali iliamua kuongeza miaka 15 bila kuweka suala hilo hadharani.

 

“TICTS kazi zao ni mbovu, lakini cha kushangaza serikali imeongeza miaka 15 zaidi katika mkataba… tena ndani ya mkataba kuna kipengele ambacho kinafanya kampuni hiyo kuwa monopoly (uhuru wa kuwa peke yake katika biashara).

 

“Kipengele hicho kinaeleza kampuni hiyo itakapokuwa na uwezo wa kuingiza kontena 600,000 kwa mwaka, ndio wataruhusiwa washindani wengine katika biashara hiyo,” alisema.

 

Alisema kipengele hicho cha mkataba kinasababisha kampuni hiyo kufanya kazi kidogo kidogo, ili wasipate washindani.

 

Mbunge huyo alishauri kipengele hicho kifutwe katika mkataba huo haraka, sambamba na kuondolewa kipengele cha ukodishwaji kwa miaka 15 iliyoongezwa katika mkataba huo.

 

Mjumbe mwingine, Mtutura Mtutura (Tunduru-CCM), alisema utendaji mbovu wa TICTS unatokana na mkataba mbovu ulioingiwa baina ya serikali na kampuni hiyo.

 

Alisema kwa kutumia kipengele cha monopoly, kampuni hiyo ina uhuru wa kuchezea huduma hiyo na aliishauri serikali kuangalia upya mkataba huo.

 

Pia alihoji kwa nini serikali iliamua kuupitia upya mkataba huo wakati muda wa awali wa mkataba huo ulikuwa haujamalizika.

 

“Tena serikali ili-renew (huisha) mkataba huo katika kipindi cha uchaguzi mkuu. Je, serikali ilikuwa na haraka gani?” alihoji Mtutura.

 

Akijibu hoja kwa wabunge hao, mmoja wa maofisa wa TICTS, alisema kwa siku bandarini wanapokea karibu kontena 60, na sehemu yenyewe ni ndogo, ndiyo maana kunaonekana kuna mlundikano wa mizigo.

 

Hata hivyo, alisema wana ghala la kuweka makontena eneo la Ubungo, lakini tatizo ni jinsi ya kuyasafirisha mpaka eneo hilo na kusema kwamba wameshazungumza na Shirika la Reli (TRL) ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

 

“Tumezungumza na mwekezaji mpya wa TRL na kuanzia Februari mwaka huu, tutaanza kupeleka kontena Ubungo, ili kupunguza msongamano,” alisema.

 

Hata hivyo, mbunge mwingine, Philemon Sarungi (Rorya-CCM), alisema TICTS haijatekeleza agizo la Waziri Mkuu, Edward Lowassa la kuwataka wapunguze mlundiko mkubwa wa makontena bandarini hapo.

 

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Dk. Batholomew Rufunjo, alisema serikali iliamua kuongeza muda wa mkataba huo kutokana na maendeleo mazuri yaliyoonekana bandarini.

 

Hata hivyo, jibu hilo liliwafanya baadhi ya wabunge kuguna na kumtaka Rufunjo kutoa sababu za msingi.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Missanga, aliingilia kati na kusema: “Watu wanahoji kulikuwa na haraka gani ya serikali kuongeza muda na mbona ilikuwa kimyakimya? Haikutangazwa?”

 

Hata hivyo, baada ya hoja hizo, alipotakiwa kujibu, Rufunjo alisema ameshaeleza sababu za kuongezwa kwa muda wa mkataba huo na kumuomba Mwenyekiti aendelee kuzungumza.

 

Malecela alisikika akisema swali hilo ni gumu na kusema kamati hiyo inahitaji kuuona mkataba huo, ili iweze kuishauri serikali baadhi ya vipengele vya kuvirekebisha.

 

Kamati hiyo iliamua kuhoji kuhusu mkataba huo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa kampuni hiyo.

 

Wakati fulani alipotembea kitengo hicho bandarini hapo, Lowassa aliagiza TICTS ifanye kazi kwa saa 24 kama njia ya kupunguza mlundikano wa makontena na kupunguza kero za wafanyabiashara.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents