Habari

Wachina wawili matatani kwa kumteka mwenzao

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia raia wawili wa China kwa tuhuma za kumteka nyara Mchina mwenzao, Liu Hong (48) ambaye ni mfanyakazi wa Le Grande Cassino, wakidai kulipwa dola za Marekani 19,000 (zaidi ya shilingi milioni 38).

dscf2219

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano hii,jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro, alisema walipokea taarifa kwamba raia huyo wa China alitekwa nyara na watu wasiofahamika.

“Oktoba 24, mwaka huu saa 11 jioni kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha polisi kanda maalumu walibaini kuwa wateka nyara hao wapo katika hoteli ya Palm Beach Upanga na walipofika hapo wakaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine,” alisema Kamanda Sirro.

Aidha kamanda Sirro alisema, “Polisi walipofika chumba namba tisa na kugonga wahusika waligoma kufungua mlango ndipo polisi waligundua wateka nyara hao kuwepo katika chumba hicho. Wakiwa wanajiandaa kuvunja mlango, mara mtuhumiwa mmoja Wang Young Jing (37) raia wa China aliamua kufungua mlango na kumkamata akiwa na Liu ambaye ni mtekwa nyara.”

“Askari walipoingia ndani walimkuta aliyetekwa nyara akiwa hajitambui akiwa na majeraha usoni. Pia katika tukio hili, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine aitwaye Chen Chung Bao (35) raia wa China ambaye ndiye aliyekodi chumba hicho,” alieleza kamanda.

“Ndani ya chumba hicho kulikutwa vipande viwili vya taulo walivyotumia kumfunga mikono, kamba za plastiki na bomba la sindano. Alisema majeruhi alipelekwa katika hospitali ya taifa Muhimbili kwa matibabu na watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa. Upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani,”aliongeza.

Alisema taarifa hizo zilieleza kwamba Liu alitekwa nyara Oktoba 23, mwaka huu saa moja asubuhi na ndipo polisi wakaunda kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini watekaji walikuwa wakidai Yen 100,000 (fedha za China) ambazo ni sawa na dola za Marekani 19,000.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents