Habari

Wadaiwa sugu wapewa siku 30 na Bodi ya Mikopo

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa siku 30 kuanzia leo Novemba 14, 2016 kwa wanufaika wa mikopo hiyo ambao imewaita “Wadaiwa Sugu” kulipa madeni yao, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
heslb-ceo-mr-badru
Abdul-Razaq Badru – Mkurugenzi Mtendaji HESLB

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo Abdul-Razaq Badru amesema kuwa hadi sasa kuna jumla ya wadaiwa sugu 142,470 wenye mikopo ya shilingi 239,353,750,170.27 iliyokwishaiva hawajajitokeza wala kuanza kulipa mikopo yao.

Akitolea ufafanuzi wa maana ya neo “Wadaiwa Sugu”, Badru amesema kuwa ni wanufaika waliokopeshwa, muda wa matarajio ukapita bila kuwasilisha taarifa zao na kulipa madeni ya mikopo waliyokopeshwa tangu mwaka wa masomo 1994/1995.

Kuhusu hatua zinazochukuliwa na bodi hiyo, Badru amesema mbali na kutoa siku 30, bodi hiyo inakamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani kwa kuvunja sheria ya bodi ya mikopo kifungu cha 19A(1).

Hatua nyingine ni pamoja na kuyawasilisha majina hayo katika taasisi za mikopo, kuwasiliana na wadhamini wao pamoja na kuyatangaza hadharani majina ya wadaiwa sugu wote ili waajiri, wadhamini na wadau wengine wayajue na kutoa taarifa katika bodi hiyo.

Kuhusu takwimu za mikopo iliyotolewa, amesema tangu 1994/95 hadi 2015/16 jumla ya shilingi 2,595,932,575.56 zimekopeshwa kwa jumla ya wanufaika 379,179.

Amesema kati ya mikopo yote iliyokopeshwa, mikopo iliyoiva ni shilingi 1,425,708,285,046.48 kwa wanufaika 238,430 ambao tayari wamemaliza kipindi chao cha matazamio.

Badru amesema kuwa jumla ya wanufaika wa mikopo 93,500 wamebainika na kupelekewa ankara za madeni yao, ambapo kati yao wanufaika 81,055 wanaendelea kulipa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents