Wadau wapingana kuhusu viingilio

Mashabiki wa soka nchini wamepokea kwa hisia tofauti viingilio vya mchezo wa kirafiki wa kimataifa baina ya Taifa Stars ya Tanzania na Selecao ya Brazil utaofanyika Juni 7, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi siku moja baada ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kutangaza viingilio hivyo, wadau  hao baadhi wamedai  ni  vikubwa mno kiasi cha kuwa kikwazo kwa Watanzania walio wengi hasa wenye kipato cha chini, wengine wakivitetea.


TFF, juzi ilitangaza kiingilio cha juu kuwa Sh200,000 na kile cha chini kikiwa Sh30,000.

Viingilio kamili vya mchezo  huo ni Sh 200,000 kwa VIP A, Sh 150,000, kwa VIP B, Sh100,000 VIP C , Sh 80,000 kwa viti vya rangi  ya chungwa, Sh 50,000 kwa viti vya rangi ya chungwa nyuma ya magoli na Sh 30,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.

Wengi wa mashabiki hao wameilalamikia serikali ambayo inamiliki Uwanja wa Taifa pamoja na TFF  kwa kupanga viingilio  vikubwa bila kujali hali za maisha za wananchi wa kawaida.

” Watanzania tulio wengi hatuwezi kulipa viingilio hivi na vimekua  kikwazo kwetu kiasi cha kuikosa mechi hiyo na nyota wa soka wa Brazil,” alieleza shabiki aliyejitambulisha kwa jina la  Victor, mkazi wa Dar es Salaam.

Shabiki huyo aliungana na wengine waliodai kuwa licha ya serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwaleta nyota hao nchini, ilipaswa kuangalia pia na uwezo wa raia na mashabiki wa soka nchini na kuweka viingilio vinavyowezekana.

“Ni ajabu, sijui kwa sababu ni Brazil, kiasi hicho cha kiingilio hakijawahi kutokea nchini kinatukatisha tamaa mashabiki  tuliokuwa na hamu ya kutazama mchezo huo.

“Kwa kweli hii ni kali hata kama tunafidia fedha ambazo zitatumika kuwaleta nchini, lakini viongozi wetu (serikalini) na TFF walipaswa kuliangalia hili kwa mapana zaidi.

Kwa haraka mashabiki wen gi wa mpira wana kipato kidogo amba cho ukiwaambia kulipa kiasi cha Shilingi 50,000 au hata hizo 30,000   itakuwa vigumu kwao na hawataweza, kwa kweli  katika hili wengi tutashindwa kuona mchezo laivu,”alisema Erick Kabendera.

Kocha wa timu ya vijana ya taifa, Rogasian Kaijage alisema ukubwa wa viingilio vya mchezo huo utawakosesha wadau wengi kuiangalia timu yao ikiandika historia kwa kucheza na Brazil, mabingwa wa kihistoria wa dunia.

Aliongeza kuwa  kuwa licha ya gharama zitakazotumika kuwaleta nchini nyota hao ambazo zimeelezwa kuwa zaidi ya Shilingi 2 bilioni, lakini serikali na TFF walipaswa kuangalia pia uwezo wa mashabiki  wengi.

“Katika hili naona litakuwa na ugumu kwa mashabiki wengi hapa nyumbani ambao kipato  chao ni kidogo, wengi  wao hawataweza kuangalia pambano hili kutokana na ukubwa wa viingilio hivyo, lakini kwa upande mwingine TFF wana haki ya kuweka viingilio hivyo vikubwa kutokana na gharama ya kuileta timu yenyewe,”alisema Kaijage.

Wadau wengine waliiambia Mwananchi  kuwa wamevutiwa  na pambano hilo na kuongeza kuwa licha ya viingilio hivyo kuonekana kuwa juu, wako tayari kwa gharama zozote  kuhakikisha hawaikosi mechi hiyo ya kihistoria ambayo imekuwa gumzo kwa  Watanzania na hata raia wa ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Mchezo huo unatarajia kuingiza Shilingi bilioni 3.6 endapo wataingia mashabiki 57,526 kulingana na idadi ya viti vilivyomo kwenye Uwanja wa Taifa.

Kabla ya kuikabili Selecao, Jumatano, Juni 7, Stars  itapambana na  Amavubi ya Rwanda kwenye mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) ambao utachezwa Juni 2. Katika mchezo wa awali, Stars walilazimishwa   sare ya bao 1-1 na Wanyarwanda hao.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents