Habari

Wafanyabiashara mihadarati sasa kufilisiwa mali zao

SERIKALI inaandaa sheria mpya ya kukabili biashara ya dawa za kulevya ambayo ikianza kazi, miongoni mwa adhabu watakazopewa watu watakaotiwa hatiani ni kutaifishwa mali zao zote.

Stella Nyemenohi


SERIKALI inaandaa sheria mpya ya kukabili biashara ya dawa za kulevya ambayo ikianza kazi, miongoni mwa adhabu watakazopewa watu watakaotiwa hatiani ni kutaifishwa mali zao zote.


Hatua hiyo inafanyika baada ya kuonekana kuwa Sheria Namba 9 ya mwaka 1995 inayotumika sasa, imekuwa ikitoa adhabu ndogo na hivyo kusababisha wahusika wa biashara hiyo, wakiwamo wafanyabiashara wakubwa, kutokuogopa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Utaratibu na Bunge), Dk. Batilda Burian, alitoa taarifa hiyo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, katika mwendelezo wa utaratibu uliowekwa kwa viongozi wa wizara kuwasiliana na umma kupitia vyombo vya habari.


Katika mkutano huo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi kutoka Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Charles Ulaya, alisema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa. Alisema mwaka huu, vigogo wapatao 128 wamewekwa chini ya uangalizi wa Mahakama na Polisi kutokana na kuhusika na biashara hiyo.


Akizungumzia sheria hiyo, Dk. Burian alisema serikali inalenga kuhakikisha mali za wahalifu hao zinataifishwa bila kujali kama zilipatikana kutokana na biashara hiyo au la.


Ingawa alisema haitaweza kuwasilishwa katika kikao cha Bunge cha Januari, lakini imepita hatua ya makatibu wakuu na sasa itajadiliwa katika Baraza la Mawaziri, tayari kwa kuiwasilisha bungeni mwaka ujao.


Akizungumzia upungufu wa sheria hiyo katika kutoa adhabu, Dk. Burian alitoa mfano kuwa inaelekeza mtu anayepatikana na hatia, kupewa ama hukumu ya faini ya Sh milioni moja au kutoa kiwango mara tatu ya mali aliyokutwa nayo.


“Lakini mahakama mara nyingi husimamia Sh milioni moja….hata unapomkamata mtu anayetumwa kusafirisha dawa, anaweza kugoma kumtaja aliyemtuma akijua kuwa kwa vyovyote vile atamtolea faini,” alisema.


Kuhusu idadi ya vigogo waliokamatwa mwaka huu, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ulaya alisema inahusisha wafanyabiashara wakubwa, wakiwamo wanaodhamini usafirishaji na uingizaji wa dawa hizo.


“Ni kweli biashara ina matajiri wakubwa wanaojulikana kama vigogo. Bahati mbaya wengine hudhani kuwa vigogo ni watu wa serikali,” alisema Ulaya na kuongeza kuwa idadi hiyo imepatikana kutokana na taarifa mbalimbali zinazotolewa na watu kwa njia mbalimbali.


Hata hivyo, anasema wakati mwingine hupata tatizo la kubaini watu wanaotajwa kwenye jamii kwa vile wanapokwenda kuwakagua, wengine hukutwa bila vithibitisho, hali ambayo ni vigumu kumchukulia hatua za kisheria.


Ulaya alisema pia serikali ina taarifa juu ya watu wapatao 13 waliokamatwa nje ya nchi mwaka huu kwa kujihusisha na biashara hiyo katika nchi za Pakistan, Uganda na Kenya.


Awali, akizungumzia mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Afrika kuhusu masuala mbalimbali ya udhibiti wa dawa za kulevya, Dk. Burian alisema Tanzania inakabiliwa na ongezeko la matumizi ya bidhaa hiyo haramu hususan bangi ambayo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka huu zilikamatwa kilo 58,058.


Hata hivyo, alisema serikali inatarajia kuunda kitengo huru cha kupambana na dawa tofauti na kikosi kazi kilichopo, kiweze kwenda sambamba na sheria mpya itakayotungwa.


Akizungumzia dawa zinazopatikana nchini, Kamishna wa Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema heroini hutoka Afghanistan wakati kokeni hutoka Marekani kupitia Afrika Kusini.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents