Habari

Wafanyabiashara waichezea Serikali

BAADA ya kubaini mchezo mchafu, Serikali imetoa siku 14 kwa kampuni 23 zilizoruhusiwa kuingiza saruji nchini kutoka nje kuhakikisha zinatekeleza jambo hilo, vinginevyo hatua zichukuliwe.

Na Said Mwishehe


BAADA ya kubaini mchezo mchafu, Serikali imetoa siku 14 kwa kampuni 23 zilizoruhusiwa kuingiza saruji nchini kutoka nje kuhakikisha zinatekeleza jambo hilo, vinginevyo hatua zichukuliwe.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Bw. Hezekiah Chibulunje, alisema hatua hiyo inatokana na kampuni hizo kushindwa kuingiza saruji licha ya kupewa vibali hivyo.


“Vibali hivyo vitafuatwa ndani ya siku 14 kuanzia leo kama kampuni hizo zitashindwa kutekeleza agizo hilo, ili kutimiza malengo ya Serikali ambayo ilikusudia kupitia kampuni hizo, kuagiza zaidi ya tani 130,000 za saruji ambazo zingesaidia kupunguza bei ya bidhaa hiyo,” alisema Bw. Chibulunje.


Alisema hadi Desemba 12 mwaka huu, saruji iliyoingizwa nchini na wafanyabiashara hao wenye vibali, ni tani 4, 701.5 kiasi ambacho ni kidogo kulinganisha na malengo yaliyowekwa.


“Wizara inafanya tathmini ya shughuli nzima ya biashara ya saruji nchini na imetoa tangazo la kuwataka wenye vibali vya kuingiza saruji kutoka nje, baada ya hapo kampuni zitakazoonekana kushindwa kuingiza saruji ndani ya muda tuliowapa, vibali vyao vitafutwa,” alisema Bw. Chibulunje.


Alisema Serikali ilipoamua kutoa vibali hivyo, ilikuwa na lengo la kujaribu kupunguza ukubwa wa tatizo la upatikanaji wa bidhaa hiyo, hivyo haioni sababu ya wenye vibali kuendelea kukaa navyo.


Akizungumzia sababu ya Serikali kutoa vibali hivyo, alisema ilitokana na tatizo lilijitokeza hivi karibuni la upungufu wa saruji nchini na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilichukua hatua za makusudi za kutoa vibali ili kukabiliana na hali hiyo.


Ilitoa vibali vya kuwawezesha wafanyabiashara kuagiza saruji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na zingine kwa lengo la kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wingi na bei nafuu.


“Wizara iliratibu shughuli ya kupokea maombi na kutoa vibali kwa wafanyabiashara mbalimbali kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa, ndipo kampuni hizo 23 zilipoonekana zinaweza kufanya kazi hiyo, lakini mambo ni kinyume, kwani wameshindwa kuingiza saruji licha ya kupewa vibali,” alisema Bw. Chibulunje.


Aliongeza kuwa bei ya mfuko wa saruji kwa sasa ni kati ya sh. 13,000 hadi sh. 25,000 kwa baadhi ya mikoa ukiwamo Mtwara. Alisema kutokana na bei hiyo, ndiyo maana wanaendelea kuwahimiza wafanyabiashara kuingiza saruji ili kuleta unafuu.


Bidhaa bandia


Bw. Chibulunje pia alizungumzia suala la kuwepo kwa bidhaa bandia katika baadhi ya maduka ambapo alisema kazi ya kuhakikisha zinaondoka, inaendelea kufanyiwa kazi kwa misingi ya sheria zilizopo.


Alisema tatizo la bidhaa bandia nchini, limesababisha matatizo mengi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wa bidhaa hizo kukwepa kulipa kodi kwa kuziingiza kinyemela.


Alisema tangu Machi hadi Oktoba mwaka huu, bidhaa bandia ziliteketezwa ikiwa ni moja ya jitihada za kupamba nazo.


Alisisitiza kuwa vita ya bidhaa hizo ni mapambano na watu wenye uwezo mkubwa kifedha, ambao kamwe hawawezi kukubali kushindwa kirahisi na kuachana na biashara hiyo.


Alisema baadhi ya watu wanaojihusisha na bidhaa bandia ni wale waliokuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya awali.


Kuhusu vipimo, alisema wizara yake inaendelea kupiga marafuku vile ambavyo si halali katika kupima bidhaa za wakulima na kukemea ujazaji kupitia kiasi kwenye magunia ya ‘lumbesa’.


Alisema vipimo hivyo vimekuwa vikiwadhulumu wakulima ambao hulazimika kuuza mazao yao kwa bei ndogo isiyolingana na vipimo vya bei.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents