Siasa

Wafanyakazi Dar waiweka Serikali mtegoni

WAFANYAKAZI mkoani Dar es Salaam wameandamana na kuipa Serikali siku 30 iwe imetangaza nyongeza mpya ya mshahara tofauti na kiwango kilichotangazwa cha sh. 84,000.

Na Reuben Kagaruki


WAFANYAKAZI mkoani Dar es Salaam wameandamana na kuipa Serikali siku 30 iwe imetangaza nyongeza mpya ya mshahara tofauti na kiwango kilichotangazwa cha sh. 84,000.


Walisema jana Dar es Salaam maandamano hayo waliyofanya ni rasharasha tu na baada ya hapo hatua zaidi zitachukuliwa.


Walitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam mbele ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Nestory Ngulla.


Wafanyakazi hao walimtaka Bw. Ngulla kufikisha kilio chao kwa Serikali na kuhakikisha anawapatia majibu katika siku 30 vinginevyo hatua nyingine itafuatia ambayo itahusisha mgomo wa wafanyakazi wa sekta binafsi na umma nchi nzima.


Akisoma risala ya wafanyakazi wa mkoa wa Dar es Salaam ambao waliandamana kuanzia Makao Makuu ya TUCTA Mnazimmoja hadi viwanja vya Jangwani, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), Bw. Evarist Mwalongo, alisema waliandamana baada ya shida kukithiri.


“Makali ya maisha hayavumiliki tena.Tunapenda kueleza kuwa Serikali imekosa huruma na kuacha kutambua wafanyakazi waliodai uhuru wakisaidiana na na wakulima,” alisema.


Alisema Serikali inawajali wafanyabiashara na kuonekana kama ndio mhimili wa kusimamia sera, uchumi na siasa za nchi. Alisema Serikali imefikia hatua ya kupuuza sheria zilizotungwa kusimamia na kulinda masuala ya wafanyakazi.


Alisema inasikitisha sana Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma chini ya Waziri Bi. Hawa Ghasia imedharau sheria namba 19 ya mwaka 2003 inayohusu majadiliano na vyama vya wafanyakazi kupanga maslahi yao.


Alisema Waziri amepuuza utawala wa sheria na kuanza ukurasa mpya kwa kupanga mishahara mpya anavyoona.
Alisema mshahara wa kima cha chini wa sh. 84,000 alioutangaza Waziri ukikatwa kodi ya sh. 600 na Akiba ya Uzeeni ya Sh. 8,400 mfanyakazi anabaki na sh. 75,000.


Alisema mshahara huo ukigawanywa kwa siku 30, mfanyakazi atalazimika kutumia sh. 2,500 kwa siku. Alisema ndio maana wafanyakazi walipendekeza walipwe kima cha chini cha sh. 315,000 kwa mwezi sawa na sh. 10,500 kwa siku.


Bw. Mwalongo alisema mshahara wa sh. 84,000 ni sawa na nusu ya posho ya mbunge anapokuwa Bungeni. Alisema kwa mwezi mbunge analipwa sh. 1,500,000 sawa na mshahara wa miezi 17.


“Uchambuzi huu ukiwekwa kwa watumishi wa sekta binafsi ambao kima cha chini ni sh.48,000 inasikitisha kiasi cha kujenga hasira mbaya katika jamii ya Watanzania,” alisema.


“Tunajiuliza ni kwa nini mapato ya nchi yanagawanywa ! Na je, wanaopewa mishahara mikubwa kiasi hicho wananunua chakula mbinguni?”Alihoji na kuongeza: “Maswali mengi yanazalishwa kutokana na pengo kubwa la kimapato lililopo.”


Alisema licha ya udogo wa mishahara, Serikali imetengeneza mzigo mzito unaotokana na bajeti ambapo bidhaa zimepanda na kumtwisha mkono mtumishi mwenye mshahara mdogo.


Wafanyakazi hao walitahadharisha mishahara isipoongezwa itakuwa ni ndoto Serikali kutokomeza rushwa. “Serikali inachochea na kushawishi rushwa idumu kwa kulipa mishahara isiyotosheleza mahitaji ya siku 30,” alisema Bw. Mwalongo.


Alisema ugumu wa maisha unapanua kiwango cha umasikini, inachochea maradhi yasiyo ya lazima, ujinga kwa sababu watu hawawezi kujiendeleza wala kusomesha watoto wao shule.


Wafanyakazi hao walisema nidhamu ya kazi haitakuwepo kwa sababu wale wenye kipato kidogo watatumia muda mwingi kupumzika hali itakayosababishwa na unyonge.


Kwa upande wake, gwiji wa sheria nchini, Prof. Issa Shivji, aliwaambia wafanyakazi hao kuwa suala la mshikamano wakati huu ni muhimu kwani kipindi tunachopita ni kigumu.


Alisema kwa kipindi cha kati ya miaka 15 na 20 imejengwa jamii yenye mgawanyiko na mpasuko mkubwa.


“Kuna kundi dogo la matajiri na kubwa la masikini…kuna matabaka ya walalakheri na walalahoi. Kama tukiendelea kwa namna hii tutakujajuta na kuna hatari ya kutokea mataifa mawili hapa nchini,” alisema na kuongeza kuwa katikati ya matabaka hayo kuna kundi la walalahai.


“Tabaka hili halina msimamo. Lina watu wanaoyumba wenye uchu wa kuingia kwa tabaka la walalakheri,” alisema.


Alisema wasomi wenzake ndio wapiga debe wa tabaka la walalakheri ingawa wapo wachache wanaoshirikiana na walalahoi.


Alisema walalahoi ndio wazalishaji na injini ya uchumi. “Lakini ni injini gani itaenda bila mafuta? Kuna haja ya kujenga mshikamano kati ya wafanyakazi na wakulima,” alisema na kuhoji kuwa tangu lini wavuja jasho wakawa masikini.


Bw. Ngulla alisema wakati umefika wafanyakazi kugombea haki zao kama ilivyokuwa wakati wa kudai uhuru.


“Lazima tuwaulize wabunge, mawaziri na Rais miaka yote wanatuonaje sisi wafanyakazi?” Alisema mshahara wa sh. 315,000 unawezekana .


Alisema mwaka 1994 walifungua kesi Mahakama ya Kazi wakidai kima cha chini kiwe sh. 84,000 na walishinda ambapo Serikali iliahidi kuwa itaanza kulipa kiwango hicho kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, lakini ilishindwa kufanya hivyo.


“Naomba tubanane nao hadi kieleweke, wafanyakazi tunayo nguvu.”Alisema Bw. Ngulla. Aliahidi kufikisha kilio chao Serikali na kuwaletea majibu kwa muda waliompa.


Maandamano hayo yalianzia makao makuu ya TUCTA kupitia barabara ya Bibi Titi, Morogoro hadi Jangwani yakishirikisha wafanyakazi waliobeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.


Baadhi ya mabango yalisomeka; “Bila walimu Rais Kikwete ungekuwa wapi?Mbona hutukumbuki? Walalahoi mshahara sh. 84,000 mbunge posho kwa siku 120,000 haki ipo wapi? Walimu tunataka mapendekezo ya mshahara wa sh.315,000,Idara ya Elimu turudishiwe posho za kufundishia. Ualimu ni kazi kama nyingine tusinyanyasike kwa lugha kuwa ni kazi ya wito.


Katika maandamano hayo wafanyakazi hao waliimba pambio mbalimbali zikiwemo za kwenye misiba. Waliimba watamlilia nani wakati wao wanazidi kukonda huku wabunge wakinawiri. Maandamano hayo yalishirikisha vyama 18 vya wafanyakazi.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents