Habari

Wafungwa 75 waachiwa huru katika gereza alilotembelea Rais Magufuli mkoani Mwanza, DPP atoa onyo kali kwa wanaobambikizia watu kesi

Ikiwa zimepita siku mbili tangu Rais Dkt. John Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Butimba Mkoani Mwanza, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, ametangaza kuwaachia huru wafungwa 325 na mahabusu katika magereza ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Image result for dpp tanzania
Biswalo Mganga

Akitoa maelezo juu ya uamuzi huo jana Julai 17, 2019 mbele ya waandishi wa habari, Mganga aliyekuwa ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Agustino Mahiga. Amesema kuwa Miongoni mwa wafungwa walioachiwa huru ni askari 8 ambao walidaiwa kupanga njama za kutorosha dhahabu kwa kushirikiana na tajiri mmoja anayeishi mkoani Mwanza.

Akitaja idadi ya wafungwa walioachiwa huru, Mganga amesema gereza la Butimba wameachiwa huru wafungwa na mahabusi 75,  Shinyanga  25, Kahama 43, Mugumu 52, Bunda 24, Bariadi 100 na Tarime 6  huku akiahidi leo atakuwa katika magereza ya Ukerewe na Sengerema.

Mganga amesema  walioachiwa huru ni wale waliobainika kubambikiwa kesi, wagonjwa, umri na tuhuma zingine zenye harufu ya rushwa kuanzia kwa raia wenyewe kwa wenyewe, mpelelezi hadi kwa hakimu, Na kusisitiza kuwa hatua ya kuwaachia ilifikiwa baada ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wahusika.

Kuhusu wafungwa waliokuwa watumishi wa umma wakiwamo askari polisi watarudishwa kazini isipokuwa kama kutakuwa na kesi nyingine ya msingi.

Natoa onyo kwa umma, mamlaka na watumishi wa umma kufanya kazi kwa maadili, mtu atakayebainika kutoa taarifa za uongo na ikabainika hivyo naomba achukuliwe hatua kali ili kuthibiti hali ya kusingiziana. Huko magerezani tumeshuhudia watoto chini miaka 18, wazee zaidi ya miaka 79, wagonjwa, walemavu ambao baada ya kuwasikiliza nimeamua kuwaondolea mashtaka na wengine kuwafutia adhabu ya kifungo,”amesema Mganga .

Kwa upande wake Waziri Dkt. Mahiga, amesema katika ziara yake Kanda ya Ziwa ndani ya siku 10, atajitahidi kutatua kero za urasimu kwa mahabusu, “Kilio kikubwa kwa wananchi ni kucheleweshwa kupata haki kutokana na upelelezi kutokamilika jambo linalosababisha magereza kujazana watu bila sababu, leo imekuwa bahati kwa gereza la Butimba maana tumekutana na Kamishna wa Magareza, DPP na mimi ndio, tumekaa wote na kuamua hivyo.” .

Waziri Mahiga na DPP wamepanga kutembelea magereza yote nchini na kuwasikiliza wafungwa na mahabusi na kutoa msamaha, Kwani Magereza yameonekana kuzidiwa na yalijengwa miaka ya 1940 .

Chanzo: Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents