Siasa

Waislamu wataka jengo lao toka Quality Group

KAMATI ya Maimamu ya Kuokoa Mali za Waislamu nchini, imeipa siku 20 kampuni ya Quality Group (1999) Limited, kurejesha kiwanja cha Waislamu kilichopo katika eneo la Chang’ombe, Wilaya ya Temeke

Na Muhibu Said


KAMATI ya Maimamu ya Kuokoa Mali za Waislamu nchini, imeipa siku 20 kampuni ya Quality Group (1999) Limited, kurejesha kiwanja cha Waislamu kilichopo katika eneo la Chang’ombe, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam na kumuomba Rais Jakaya Kikwete kuifutia kampuni hiyo umiliki wa kiwanja hicho.


Akizungumza na waandishi wa habari katika Msikiti wa Mtoro, jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati hiyo, Sheikh Khalifa Khamisi, alisema wamefikia hatua hiyo kwa kuwa kiwanja hicho ni mali halali ya Waislamu waliyopewa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kujenga Chuo Kikuu na Mwalimu mwenyewe aliomba msaada kwa Rais (wa zamani) wa Misri, Gamal Abdel Nasser ili kufanikisha azma hiyo.


Sheikh Khalifa alisema kiwanja hicho chenye ukubwa wa ekari 9.5 kinachomilikiwa kwa hati namba ID/195976, baada ya kukabidhiwa Waislamu, kilisajiliwa kwa jina la taasisi ya Muslim University of Tanzania iliyo chini ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata).


Hata hivyo, Sheikh Khalifa alisema baadaye, wadhamini wawili wa Bakwata walisaini mkataba na Quality Group (1999) Limited wa uendelezaji wa kiwanja hicho.


Alisema, katika mkataba huo uliotiwa saini Oktoba 4, mwaka 2002, Quality Group (1999) Limited ilikubaliana na Bakwata kwamba, ingejenga katika kiwanja hicho hospitali na shule ya msingi ambazo zingekuwa mali ya Bakwata na ujenzi wa vyumba vya madarasa ungekuwa umekamilika ndani ya miezi sita.


Alisema pia walikubaliana kwamba Bakwata ingekabidhi sehemu ya kiwanja kuwa miliki halali ya kampuni hiyo na kwamba, mara mradi wa ujenzi wa shule ungekamilika, kila upande ungebaki na miliki yake halali na uhusiano wa kibiashara kati yao ungekuwa umekoma.


Sheikh Khalifa alisema baada ya makubaliano hayo kufikiwa, kampuni hiyo ilipata hati ya kumiliki kiwanja hicho Desemba 8, mwaka 2003, lakini hadi sasa hakuna mahali popote katika kiwanja hicho palipojengwa hospitali wala shule ya msingi, kinyume na makubaliano yaliyofikiwa baina yao.


Alisema pamoja na hali hiyo, Mei 25, 2004 kampuni hiyo ilipewa kibali cha kuzungusha uzio katika kiwanja hicho na Februari 18, mwaka jana kibali hicho kikaidhinishwa na Manispaa ya Temeke. “Wakati huo Bakwata haikuwa imepokea hata shilingi moja kutoka kampuni hiyo,” alisema Sheikh Khalifa.


Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Maimamu ilimwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli kumuomba ahakikishe kiwanja hicho kinarudi kwa Waislamu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaban Simba akiongozana na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, walitoa msimamo wa baraza mbele ya waziri huyo wakitaka serikali kukirejesha kiwanja hicho mikononi mwake.


“Msimamo huo ulitolewa baada ya Waziri kuitaka Halmashauri Kuu ya Bakwata kutoa msimamo wake juu ya umiliki wa kiwanja hicho.


Baada ya kimya cha muda mrefu serikali imekataa kuifuta hati aliyopewa Quality Group (1999) Limited na badala yake Bakwata imepokea fedha kidogo kutoka kampuni hiyo. Tarehe 31/5/2007 Bakwata iliingiza katika akaunti yake hundi yenye thamani ya Sh86,740,000 kutoka kampuni hiyo kama kifuta jasho, baada ya serikali kukataa maombi ya Waislamu wa nchi nzima,” alisema Sheikh Khalifa.


Alipoulizwa jana na Mwananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Taifa ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka, alikiri Bakwata kuingiziwa fedha hizo katika akaunti yake.


Kutokana na hali hiyo, Sheikh Khalifa aliitaka kampuni hiyo kwenda kuchukua fedha ilizoipa Bakwata, akisema kuwa mkataba uliosainiwa na baadhi ya viongozi wa Bakwata na kampuni hiyo kuhusu mauzo ya kiwanja hicho, haukuzingatia maslahi ya umma wala shabaha ya serikali kutoa kiwanja hicho.


“Ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona kwamba serikali iliyochaguliwa na umma kwa manufaa ya umma licha ya kuahidi kupitia Waziri Magufuli kutekeleza maombi ya umma wa Waislamu wa Tanzania nzima, imeyapuuza maombi yao ili kulinda maslahi binafsi ya mfanyabiashara mmoja,” alisema Sheikh Khalifa.


Juhudi za kumpata mmiliki wa Quality Group, Yusuf Manji ziligonga mwamba baada ya msaidizi wake kudai kuwa yuko nje ya nchi.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents