Wakuu wa shule zinazofanya fujo sasa kutimuliwa

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema kuanzia sasa mkuu wa shule ambaye wanafunzi wake watafanya vurugu atafukuzwa kazi

MWandishi wa Habari Leo 


 


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema kuanzia sasa mkuu wa shule ambaye wanafunzi wake watafanya vurugu atafukuzwa kazi.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mwantumu Mahiza alisema jana kuwa vurugu katika sekondari za serikali zinasababishwa na kutowajibika kwa wakuu wa shule hizo ambao alidai wengi wanapoteza muda mwingi kuwa safarini.

“Hatutaki kusikia tena migogoro shuleni, tukisikia vurugu hapo mwalimu haponi,” alisema Mahiza na kuongeza, “hatuwezi kufukuza tu wanafunzi, sasa tunawageukia ninyi walimu.”

Naibu Waziri huyo alisema suala la vurugu shuleni linawakosesha raha na kuwapotezea amani watendaji wa wizara hiyo, kwani shule ni kiwanda cha kutengeneza wataalamu wa baadaye.

Mahiza alikuwa akizungumza na Sekretarieti ya Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) katika Shule ya Sekondari Jangwani, Dar es Salaam.

Aliwataka walimu wakuu hao kujiuliza nini chanzo cha vurugu, nini kinawashinda walimu hao kuwalea wanafunzi hadi waharibu mali na kama wanawajibika katika shule zao.

Alisema wanafunzi hawawezi kukurupuka tu kufanya vurugu na kugoma lazima kuna msigano kati yao na uongozi wa shule. Alisema walimu hao pia wajiulize kama wanawashirikisha wanafunzi katika maamuzi ya maisha yao pale shuleni na pale wanapotaka kufanya mabadiliko.

Alisema maswali hayo yawe dira katika utendaji wao wa kila siku ili kuhakikisha vurugu hizo zinakoma mashuleni. Alisema wakuu wa shule hizo pia wajihoji aina ya utawala wanaoutumia kama ni wa kibwanyenye au ni ule wa kila mtu la lake.


“Badilisheni aina ya utawala wenu, mnapenda kukasimu madaraka na nyinyi muda mwingi mnautumia safarini,” alisema Mahiza na kuwaagiza walimu hao kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utendaji katika maeneo yao ya kazi.

Alisema moja ya matatizo yanayolalamikiwa na wanafunzi ni ufundishaji usiofaa, hivyo akawataka wakuu wa shule kusimamia suala hilo ili walimu wafundishe kwa kufuata kanuni za ufundishaji.

Alisema wanafunzi hawakwenda shule ili waende pikiniki wala kufanya utumwa shuleni badala yake wamekwenda ili waweze kufundishwa. “Kuweni wakali katika hilo shiko liwe shoko na kalamu iwe kalamu, anayeona ualimu hauwezi aondoke,” alisema Naibu Waziri huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu.

Kuhusu chakula, Mahiza alisema hilo ni tatizo kubwa hivyo amewataka wakuu hao wa shule kutumia asilimia 50 ya ada za wanafunzi kwa ajili ya chakula. Pia aliwataka wawe wawazi kuwashirikisha wanafunzi katika suala la chakula kutokana na mapato yaliyopo shuleni.

Lakini alisema kuwapo kwa usiri katika suala hilo kunakofanywa na baadhi ya wakuu wa shule kumechangia wanafunzi kutokuwa na imani na uongozi, hali inayochangia kutokea kwa migomo na vurugu mashuleni.

Pia amewaagiza walimu walezi kukaa na wanafunzi ili kufahamu wanakotoka wapi na wajue namna ya kuwasaidia. Aliwaagiza wakuu hao kurudisha misingi ya ualimu katika shule zao, jambo alilodai iwapo litafuatwa migogoro itamalizika.


 


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents