Habari

Walimu wasema: Heri wakati wa ‘Mkoloni’

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema mshahara waliokuwa wakilipwa walimu nchini kati ya miaka ya 1960 na 1980 ilikuwa mikubwa na yenye kutosheleza tofauti na ya sasa.

Na Nickson Mkilanya, Morogoro

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema mshahara waliokuwa wakilipwa walimu nchini kati ya miaka ya 1960 na 1980 ilikuwa mikubwa na yenye kutosheleza tofauti na ya sasa.

Rais wa CWT, Bw. Gratian Mukoba, alisema mjini hapa hivi karibuni katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi na kubainisha kuwa ari ya ufundishaji na kujitolea ilikuwa kubwa kwa walimu kote nchini wakati huo.

Bw. Mukoba alisema mshahara huo unaonekana kuwa mkubwa ikilinganishwa na sasa kwa kuwa fedha kidogo walizokuwa wakilipwa walimu miaka ya nyuma zilikuwa zinaweza kutosheleza mahitaji yote ya msingi ya mwalimu.

Alifafanua kuwa kiwango hicho cha mshahara wa miaka ya sitini ni tofauti kabisa na sasa, kwa kuwa mshahara wa sasa wa walimu ni mkubwa, lakini usioweza kutosheleza mahitaji ya msingi, hali ambayo pia inachangiwa na kupanda kwa gharama za maisha nchini.

“Sasa ukweli ni upi kama si huo kwamba miaka ya sitini hadi themanini mshahara wa walimu ulikuwa mkubwa sana ukilinganisha na sasa, kwani sasa hivi fedha za mshahara ni nyingi kwa kuhesabu, lakini ni kidogo kwa matumizi kwa kuwa gharama za maisha zimepanda, huku mishahara ni ile ile,” alifafanua Bw. Mukoba.

Alisema njia za kumaliza tatizo hilo ni Serikali kuona jinsi ya kutoa mishahara inayokwenda na maisha ya sasa, ili pamoja na kusaidia juhudi za walimu za kupambana na umaskini, lakini pia hali hiyo itaongeza morali ya ufundishaji kwa walimu nchini.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents