Waliokufa Kenya sasa zaidi ya 560

IDADI ya watu wanaokufa kutokana na vurugu zinazoendelea nchini Kenya kwa siku ya nne mfululizo hadi kufikia jana zaidi ya watu 560 wamepoteza maisha yao nchini humo.

Tausi Mbowe na Mashirika ya Habari


IDADI ya watu wanaokufa kutokana na vurugu zinazoendelea nchini Kenya kwa siku ya nne mfululizo hadi kufikia jana zaidi ya watu 560 wamepoteza maisha yao nchini humo.


Wakati serikali ikitangaza kuwa wastani wa watu 300 wamepoteza maisha katika ghasia hizo, Chama cha Orange Democratic Change (ODM), kimesema kuwa hadi juzi watu 500 wamefariki katika mapigano hayo katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo. Taarifa zingine zilizopatikana jana zimesema kuwa idadi ya watu waliokufa baada ya kanisa kuchomwa moto huko Eldoret juzi imeongezeka kutoka watu 40 hadi 100 ikiwa ni ongezeko la watu 60 zaidi ya wale walioelezwa kufariki juzi.


Ghasia hizo ambazo sasa zimeonyesha kuchukua sura tofauti ya ukabila kati ya Kikuyu dhidi ya Wajaluo na makabila mengine yaliyosababisha mauji ya watu wa rika mbalimbali. Kenya ina zaidi ya makabila 40.


Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya jana ilisema kuwa mpaka kufikia jana jioni zaidi ya watu 300 walipoteza maisha katika vurugu hizo ambazo kwa siku ya jana zilionekana kupungua katika baadhi ya maeneo.


Hata hivyo, ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, kimesema kuwa idadi iliyotangazwa na serikali pamoja na Mashirika ya Kimataifa si sahihi na kwamba mpaka sasa zaidi ya watu waliouawa katika ghasia hizo ni 500.


Hata hivyo, wakati Mashirika ya Kimataifa na ODM vikitoa idadi kumbwa ya watu waliouawa katika machafuko hayo, vyombo vya habari vya nchi hiyo vimekuwa vikiripoti idadi ndogo sana na hadi kufikia jana vyombo hivyo viliripoti kuwa ni watu 164 walikuwa wameuawa katika ghasia hizo Mjini Eldoret ambako Kanisa la Assemblies of God lilichomwa moto na kusababisha jumla ya watu 40 kupoteza maisha, inasemekana idadi hiyo iliongezeka na kufikia watu 100.


Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), idadi ya waliopoteza maisha hadi kufikia jana iliongezeka na kufikia watu 100 kutokana na watu hao kupata majeraha makubwa yaliyosababishwa na moto huo. Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera, juzi kilionyesha watu zaidi ya watu 40 wakiuawa kwa kuchomwa moto ndani ya kanisa hilo walimokimbilia kuepuka ghasia mitaani. Inakadiriwa jumla ya watu 400 walikuwa ndani ya kanisa hilo.


Maafisa wa polisi na watu walioshuhudia tukio hilo walisema watu hao walichomwa moto wanaodhaniwa kuwa ni kutoka kabila la Kikuyu analotoka Rais Mwai Kibaki waliokimbilia kanisani humo kujificha kuepuka ghasia mitaani.


Katika tukio hilo, watu kadhaa walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kutibiwa majeraha makubwa ya moto waliyoyapata baada ya kunusurika kifo. Pia jana baadhi ya vijana walichoma Kanisa jingine, jijini Nairobi, lakini haikujulikana mara moja kama uchomaji huo wa kanisa ulisababisha vifo.


Katika tukio jingine, Daktari wa Hospitali ya Taifa ya Nairobi, John Okello alisema kuwa zahanati zote za jijini Nairobi zimekumbwa na upungufu mkubwa wa vifaa kama �gauze� kutokana na kupokea wagonjwa wengi kuliko uwezo wake.


Dk Okello alisema ili kukabiliana na tatizo hilo hospitali yake inajaribu kusambaza vifaa hivyo kwa zahanati hizo kutokana na idadi kubwa ya majeruhi. Wengi wa wagonjwa wanaopelekwa hospitali wana majeraha ya kukatwa na mapanga.


Ghasia hizo zinazoendelea kwa siku nne mfululizo sasa nchini Kenya pia zimesababisha zaidi ya watu 75,000 kukosa mahali pa kuishi kufuatia nyumba zao kuchomwa moto katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.


Hali katika jiji la Nairobi jana ilikuwa shwari huku baadhi ya maduka yakifunguliwa katika meneo mbalimbali polisi wakiwa wame imarisha ulinzi mkali katika maeneo hayo. Msemaji wa serikali ya Kenya, Alfred Mutua alisema idadi ya watu walioathirika na mapigano hayo ni ndogo sana na kuifananisha sawa na asilimia tatu tu ya idadi ya Wakenya wote wanaofikia milioni 34 na kuongeza kuwa si kila upande wa Kenya umekubwa na machafuko hayo.


Mutua alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi linawashikili jumla ya watu 500 kwa kujihusisha na mapigano hayo tangu kuanza kwa ghasia hizo katika sehemu mbalimbali. Katika tamko lao la pamoja Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Condoleezza Rice na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Miliband walizitaka pande zinazovutana kuhakikisha wanakaa pamoja ili kuzungumza tofauti zao ili hali ya amani ipatikane nchini humo kwa maslahi ya wananchi wa Kenya. Hata hivyo mawaziri hao kutoka mojawapo ya mataifa makubwa duniani walisema kuwa kulikuwa na kasoro kubwa katika kutangaza kwa matokeo hayo.


Umoja wa Nchi za Afrika ulimtuma Rais wa Ghana John Kufuor, kwenda nchini Kenya kukutana na pande zote zinazopingana ili kuhakikisha hali ya amani inapatikana katika nchi hiyo. Awali Msemaji wa Umoja huo Habiba Mejri-Cheikh alisema Kufuor atawasili nchini Kenya siku ya Jumatano (jana), hata hivyo Ofisi ya Habari ya rais Kufuor ilisema kuwa rais huyo ameahirisha safari hiyo.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Akwasi Osei-Adjei alisema raisi Kufuor anasubiri kufanya mazungumzo ya simu kwanza na rais Kibaki kabla hajaamua kama atatuma mwakilishi wake wa Afrika Mashariki au kwenda yaye mwenyewe.


“Bado hatujasikia kutoka kwa rasi Kibaki, rais Kufuor ameshafanya mazungumzo na kiongozi wa ODM Odinga, na hili kuwa sawa katika kusimamia hali hiyo ni vizuri kuongea na pande zote mbili kabla ya kwenda moja kwa moja kuonana nao,� alisema Osei-Adjei wakati anazungumza na Shirika la Habari la Reuters.


Hata hivyo, ODM imesisitiza azma yake ya kuendelea na maandamano yake ya amani waliyopangwa kufanyika leo licha ya Jeshi la Polisi kupinga kufanyaika kwa maandamano hayo. Juzi kiongozi wa chama hicho, Odinga wa ODM aliitisha maandamano makubwa ya amani kwa wafusi wake na kutaka yafanyike katika viwanja vya Uhuru Park kwa kile alichodai kupinga matokeo yaliyompa ushindi rais Kibaki.


Chama hicho jana kilipokea barua kutoka jeshi la Polisi likizua kufanyika kwa maandamano hayo, lakini viongozi wake walisisitiza kuwapo kwa maandamano kwa usalama tu na si kuzuia maandamano hayo.


Kutokana na watu wengi kukaa katika nyumba zao kwa kuhofia madhara ya ghasia hizo hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na wananchi hao kukosa chakula na maji. Katika hatua nyingine, habari kutoka Kenya zilisema kwamba Rais Kibaki jana jioni alitarajiwa kukutana na wabunge wa upinzani, lakini Odinga alisema hawezi kukutana na Rais Kibaki.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents