Wallace Karia achukua fomu kuwania Urais Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati 

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amejitokeza kuwania Urais wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), ambalo linatarajia kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Desemba 18, mwaka huu jijini Kampala nchini Uganda.

Image result for wallace karia

Akizungumza na gazeti Nipashe jana, Karia, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuombwa na marais wenzake wa nchi wanachama na kuamini ana uwezo wa kutoa mchango wake katika kuongoza baraza hilo.

Karia alisema anaamini akichagulia kuliongoza baraza hilo, atahakikisha malengo ya Cecafa yanakamilika, ikiwamo kupandisha viwango vya nchi wanachama.

“Nimeshajaza fomu na kuirudisha, na kama nitakuwa mgombea peke yangu, basi sitapigiwa kura, mkutano mkuu utaniidhinisha moja kwa moja, naamini marais wenzangu, hawatanigeuka, kwa sababu wameshaonyesha kuniamini,” alisema

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alisema mbali na nafasi ya urais, alitaja nafasi nyingine zitakazowaniwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na Wajumbe watatu watakaounda Kamati ya Utendaji.

Musonye alisema tayari nchi wanachama wa Cecafa wameshaanza maandalizi ya kuelekea katika mchakato huo, ambao anaamini utaongeza nguvu katika utendaji.

Alizitaja nchi wanachama zitakazoshiriki katika uchaguzi huo kuwa ni pamoja na Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somalia, Sudan na Sudan Kusini.

Uongozi mpya utakaoingia madarakani, ndio utamteua Katibu Mkuu mpya ambaye atarithi mikoba ya Musonye, ambaye ametangaza kustaafu kiti hicho ifikapo Juni mwakani.

Musonye amekaa madarakani katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka 20, akifanya kazi na marais watano akiwamo Leodegar Tenga wa Tanzania na Mutasim Gafaar kutoka Sudan ambaye anamaliza muda wake.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW