Habari

Wanafunzi Chuo Kikuu Dodoma kuishi gesti

WANAFUNZI watakaojiunga na Chuo Kikuu kipya kitakachofunguliwa hapa Septemba mwaka huu, wanakabiliwa na uwezekano wa kulala katika nyumba za wageni ambazo hivi sasa zinageuzwa hosteli, imefahamika.

Martha Mtangoo, Dodoma

 

WANAFUNZI watakaojiunga na Chuo Kikuu kipya kitakachofunguliwa hapa Septemba mwaka huu, wanakabiliwa na uwezekano wa kulala katika nyumba za wageni ambazo hivi sasa zinageuzwa hosteli, imefahamika. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, William Lukuvi aliyaeleza hayo alipozungumza na uongozi wa chuo kikuu hicho kipya jana.

 

Alisema kwa sasa zaidi ya nyumba za kulala wageni 51 mjini hapa zimekwisha kugeuzwa hosteli za wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo cha Mipango, hali ambayo inaaminika ndiyo itakayowakabili wanafunzi wa chuo kikuu hicho kipya. Lukuvi alisema jambo hilo linautia aibu mkoa wake kutokana na nyumba hizo kufanywa hosteli za kulala wanafunzi badala ya vyuo husika kujenga hosteli.

 

Alisema kwa sababu hiyo, kuna tishio la nyumba zote za kulala wageni mjini hapa kuwa hosteli kutokana na uanzishwaji wa vyuo vikuu vipya viwili ambavyo vinatarajiwa kuanza mwaka huu. Lukuvi aliyataka mashirika na watu binafsi kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi na hivyo kupanua mji wa Dodoma ambao muda mfupi ujao utakuwa kitovu cha elimu nchini.

 

Baadhi ya nyumba za kulala wageni ambazo zimegeuzwa hosteli ni Morning Star, Bonanza, Enugu, CCT, Mapambazuko na Furaha. Wanafunzi wanaoishi humo wanasema mazingira wanayoishi ni mazuri ingawa mchana huwa kunakuwa na kelele na hakuna utulivu. Nyumba hizo pia hazina sehemu za kupumzika na kufanya michezo na mazoezi.

 

Wakati huohuo, Lukuvi amewataka wote ambao si wafanyakazi wa serikali lakini wanaishi katika nyumba za serikali kuondoka mara moja na kuwaachia walengwa. Alisema kuna wafanyabiashara wakubwa wanaoishi katika nyumba za serikali ambazo wamekuwa wakilipa fedha kidogo huku nyumba zao wakipangisha na kutoza kodi kubwa.

 

Lukuvi alisema kuna baadhi ya watumishi wa serikali ambao wamekuwa wakiishi katika nyumba za kupanga wakati nyumba wanazotakiwa kuishi zina watu ambao si walengwa. “Sitaki kuwaona watu wa kawaida wanaishi katika nyum a za serikali, waondoke na hizo nyumba zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo,” alisema.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents