Habari

Wanafunzi shule ya msingi waoa

Baadhi ya wanafunzi wa kiume na wanaosoma Shule ya Msingi ya Karamba iliyoko kijiji cha Toloha kata ya Kwakoa wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wamefungishwa ndoa za kimila na wazazi wao.

Na Asraji Mvungi, PST, Mwanga

 
Baadhi ya wanafunzi wa kiume na wanaosoma Shule ya Msingi ya Karamba iliyoko kijiji cha Toloha kata ya Kwakoa wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wamefungishwa ndoa za kimila na wazazi wao.

 

Wakizungumza na PST shuleni hapo, baadhi ya wananchi na walimu wa shule hiyo walisema wanafunzi hao wanaozeshwa wakiwa bado shuleni ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mila na desturi za kabila la wafugaji wa jamii ya Kimasai.

 

Hata hivyo, wananchi hao walisema hawaoni tatizo kwa wavulana wa shule ya msingi kusoma wakiwa wake nyumbani.

 

Sheria ya elimu nchini inawazuia wanafunzi wanaosoma shule za msingi na sekondari kuoa au kuolewa.

 

Wananchi wa kijiji hicho kilichoko mpakani mwa Tanzania na Kenya walisema kwa mujibu wa mila na desturi za kabila hilo vijana wa kabila la wafugaji wanaruhusiwa kuoa mara tu baada ya kutairiwa.

 

Mwalimu wa shule hiyo, Bw. Isack Mndeme alimweleza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe aliyetembelea kata hiyo kuwa pamoja na vijana wa jamii hiyo kuoa wakiwa shuleni pia lipo tatizo la wanafunzi wa kike kukatishwa masomo kwa sababu ya kuolewa.

 

Alisema pamoja na jitihada za serikali za kuhamasisha uandikishaji wa watoto na kufanikiwa kuandikisha idadi kubwa ya wasichana, wengi wao hawamalizi darasa la saba kwa sababu hizo.

 

“Wanafunzi wengi wasichana hawamalizi shule kwa sababu wanaolewa mapema, pamoja na wananchi hawa kujitahidi katika uandikishaji wa wanafunzi, wanapofika darasa la tano ama la sita tayari wanakuwa ni wake za watu, na wanaanza kutoroka kidogo kidogo na tukifuatilia tunaambiwa wamehama,“ alisema mwalimu.

 

Aidha mwalimu huyo alisema hata wanafunzi wa kiume wamekuwa wakioa wakiwa bado wanasoma japo kwa upande wao wamekuwa wakiendelea na masomo kama kawaida.

 

Alisema kutokana na hali hiyo idadi ya wanafunzi wa kike wanasoma katika shule hiyo ni wachache mno ikilinganishwa na wavulana.

 

Wakizungumzia utaratibu wa vijana wao kuoa bado wakiwa shuleni baadhi ya wananchi wa jamii hiyo pamoja na kukiri kuwepo hali hiyo walisema hawajaona kuwa ni tatizo kwani kimsingi vijana wao wanapata elimu na hapo hapo wanakuwa wamedumisha mila.

 

“Ni kweli kuwa kuna baadhi ya vijana wanaoa bado wakiwa shuleni lakini hakuna tatizo kwani elimu wanapata na pia mila wanadumisha,“ alisema mmoja wa wananchi hao.

 

Hata hivyo, baadhi ya wazee wa mila wa kabila la wafugaji hao wa Kimasai walisema kuwa tatizo hilo linachangiwa na uelewa mdogo wa wananchi wengi wa jamii hiyo wa juu ya umuhimu wa elimu.

 

Walisema pia umbali wanaotembea wanafunzi hao kutoka nyumbani hadi shuleni unachangia wanafunzi wengi kutoroka ama kukatishwa masomo.

 

“Ni kweli hili ni tatizo lakini kwa kiasi kikubwa linachangiwa na wazazi wengi kutoelewa maana na umuhimu wa elimu, na tunataka tuombe elimu zaidi itolewe kwa wazazi kwani ndio njia pekee ya kumaliza tatizo hili,“ alisema Bw. Palesio Nalio

 

Aidha kiongozi huyo wa mila aliiomba serikali na wadau wengine kuangalia uwezekano wa kuanzisha madarasa ya elimu ya watu wazima kwa ajili ya kuwasomesha wazazi na kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi na akafafanua kwamba wako tayari kuchangia.

 

“Unajua hili tatizo linatokana na wazazi wengi kutopata elimu, hapa dawa ni kuwasomesha kwanza hawa wazazi kupitia elimu ya watu wazima na kujenga hosteli na hili tutakuwa tayari kuchangia,“alisema.

 

Akizungumzia suala hilo Waziri wa Elimu, Profesa Jumanne Maghembe aliwataka wananchi hao kuacha tabia ya kuoa na kuwaozesha watoto wadogo kwa kisingizio cha mila.

 

Alisema pamoja na serikali kutambua na kuheshimu mila na desturi za wananchi wake haikubali kuona zikitumika vibaya na kuendelea kuwaathiri watoto na hasa watoto wa kike.

 

“Hapa katika shule yenu wanafunzi wa kike ni wachache mno sio kweli kuwa hawapo, wapo lakini mmewaoa… Jamani acheni kuoa watoto, acheni wakue, wasome ndipo muwaoe,“ alisema Profesa Maghembe.

 

Aidha aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kuangalia namna ya kutokomeza tatizo hilo haraka iwezekanavyo na kuhakikisha kwamba wanafunzi wa jamii hiyo hasa wasichana wanapata elimu kama walivyo watoto wa Watanzania wengine.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents