Habari

Wanafunzi vyuo vikuu vitano wafukuzwa

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiondoka katika maeneo ya chuo baada ya Serikali kukifunga jana. (Picha na Athumani Hamisi).Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umetangaza kukifunga chuo hicho kwa muda usiojulikana na kuwatimua wanafunzi wote baada ya kukaidi agizo la kuwataka warejee madarasani

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiondoka katika maeneo ya chuo baada ya Serikali kukifunga jana. (Picha na Athumani Hamisi).Oscar Mbuza na Shadrack Sagati


Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umetangaza kukifunga chuo hicho kwa muda usiojulikana na kuwatimua wanafunzi wote baada ya kukaidi agizo la kuwataka warejee madarasani. Uamuzi huo ulitokana na kikao cha Baraza Kuu la chuo hicho lililoamua kufunga chuo hicho pamoja na vyuo vyake vishiriki baada ya juhudi za kuwabembeleza wanafunzi hao kushindikana.


Wanafunzi hao waliendeleza mgomo ulioanza juzi, pamoja na kufanya maandamano katika maeneo ya chuo.


“Tumewataka warejee makwao na wawe wameondoka maeneo ya chuo ifikapo saa 12 jioni,”(jana), alisema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala alipozungumza na gazeti hili. Wanafunzi waliofukuzwa ni wa sehemu ya Mlimani, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Chang’ombe (DUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS) na Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC).


Tangazo la kufukuzwa kwa wanafunzi hao lilitolewa jana alasiri na Ofisi ya Uhusiano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam likiwataka wanafunzi wote wawe wameondoka maeneo ya vyuo kufikia saa 12 jioni. Kufukuzwa kwa wanafunzi hao kunavuruga ratiba ya chuo hicho na sasa kitafunguliwa tena baada ya kufanyika kwa kikao cha wakuu wa vitivo, wakuu wa taasisi za chuo hicho ambao watapanga ratiba upya.


Prof. Mukandala alisema uongozi umechukua hatua ya kukifunga chuo hicho kwa sababu za usalama ikizingatiwa baadhi ya wanafunzi ambao hawako katika mgomo wamekuwa wakibughudhiwa na wenzao.


“Tumeona kwa usalama tufunge chuo baada ya vurugu na maandamano kuongezeka na hali ya wanafunzi waliogoma kuwalazimisha ambao hawakuwa kwenye mgomo nao wagome,” alisema. Wanafunzi hao wamekuwa katika mgomo tangu juzi kama njia ya kuibana Serikali iwakopeshe asilimia 100 badala ya asilimia 60 ya sasa hivi wanayolipiwa na Bodi ya Mikopo.


Kwa mujibu wa wanafunzi hao, wanadai kulipiwa kiasi hicho ili waweze kumudu gharama za mafunzo kwa vitendo, matibabu na ada.


Awali, jana asubuhi Prof. Mukandala alizungumza na waandishi wa habari na kusema uongozi wa chuo hicho ulikuwa umetoa mapendekezo ya kufungwa kwa chuo hicho baada ya jitihada za kuwabembeleza wanafunzi kurejea madarasani kugonga mwamba. “Tumejitahidi kwa namna zote, hata wenzetu wa UDASA ( Chama cha Walimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) pia wamejaribu kuwabembeleza wanafunzi, lakini wameshindwa,” alisema.


Alisema awali uongozi wa chuo uliwataka wanafunzi hao wawe wameingia madarasani hadi saa 11 jioni juzi, lakini wanafunzi hao walikaidi agizo hilo na uongozi uliendelea kuwaagiza kuwa wawe wameingia madarasani hadi saa 10 jioni jana, lakini pia waligoma. “Kwa mujibu wa sheria ndogo za chuo, wanafunzi wanapogoma kuendelea na masomo ni lazima chuo kifungwe ili kulinda hali ya usalama kwa wanafunzi wenyewe, mali za chuo na viongozi wengine,” alisema Prof. Mukandala.


Alisema uongozi wa chuo uliwaomba wanafunzi kuendelea na masomo kwa kujua kwamba madai yao yangetatuliwa Agosti mwaka huu kutokana na ahadi iliyotolewa na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, hivi karibuni.


Jana asubuhi katika eneo la Mlimani, wanafunzi hao waliendelea kuandamana kutoka eneo la majengo ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS) kuelekea majengo ya utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti tofauti. Wanafunzi hao pia walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali, nyingi zikieleza msimamo wao wa kuendelea kugoma na kutamka kwamba wapo tayari kufukuzwa chuoni hapo kama Serikali haitatoa tamko kuhusiana na madai yao.


Wakati hali ilikuwa hivyo katika vyuo hivyo viwili, wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUSCH) na wale wa Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC), kwa siku nzima jana walikuwa wanaendelea na masomo yao kama kawaida.


Naye John Nditi anaripoti kutoka Morogoro kuwa wanafunzi 2,500 wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameungana na wenzao wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mgomo kwa muda usiojulikana.


Pia katika mgomo huo umechangiwa na kupinga maamuzi ya utawala wa chuo hicho kutokana na barua yake yenye kumbukumbu namba SUA/ ADM/ H.1/ 18 ya Aprili 2, mwaka huu iliyotamka kuwa wanafunzi hao hawatapewa matokeo yao ya mitihani wasipolipa asilimia 40 na pia hawatapokelewa chuoni hapo katika muhula wa tatu.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents