Habari

Wanafunzi wakumbwa na mapepo shuleni

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Imesela, iliyopo Kata ya Imesela, Wilaya ya Shinyanga, wamekuwa wakipiga kelele shuleni bila sababu huku taarifa zilizopatikana shuleni hapo Jumatano hii zinasema kwamba, wanafunzi hao wamekuwa wakianguka na kupiga kelele, tangu Januari mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, walimu wa shule hiyo wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwatuliza na hivyo kupoteza muda wa kuingia madarasani. Mwalimu Mkuu wa shule hiyo yenye wanafunzi 252, Seleman Kalavina, alithibitisha uwepo wa tukio hilo na kusema wanafunzi kila wanapoanguka, huwa wanapiga kelele na kutamka maneno yasiyoeleweka.

Alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwemo kuwaita viongozi wa dini, lakini tatizo hilo bado halijatatuliwa.”Hali hii inatutisha hata sisi walimu kwani hatufundishi kwa vile tunatumia muda mwingi kuzima mapepo. Umefika wakati walimu wanatamani kuhama katika shule hii.”

“Kwa ujumla, hali hii inawakumba wanafunzi wa kike peke yao na mauzauza huanza kila siku saa moja na nusu asubuhi mpaka muda wa masomo unapomalizika mchana,” alisema mwalimu mkuu huyo alipokuwa akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya waliotembelea shule hiyo.

Naye Mratibu wa Elimu, Kata ya Imesela, Julius Wamba, alisema mauzauza katika shule hiyo yameongezeka kuanzia Machi mwaka huu. “Hali imezidi kuwa mbaya kuanzia Machi mwaka huu na watoto wanapokuwa wakipiga kelele, huwataja baadhi ya watu wanaowasababishia hali hiyo,kutokana na hali hiyo, tumeshaita masheikh na walokole, lakini wakiondoka tu, mapepo yanawarudia tena na wanafunzi wanashindwa kusoma.”

Na Emmy Mwaipopo

Chanzo: Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents