Habari

Wanajeshi 7 wa Umoja wa Mataifa kutoka mataifa haya wauawa nchini DR Congo

Wanajeshi 7 wa Umoja wa Mataifa kutoka mataifa haya wauawa nchini DR Congo

Umoja wa Mataifa umesema walinda wake amani wapatao 7 wameuawa katika mapigano yaliyozuka karibu na mji wa Beni kaskazini mwa Kivu, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Ni eneo lililoathiriwa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo. Bado haijajulikana ni kundi gani la waasi limehusika na mashambulizi.

Kwa mujibu wa BBC, Akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya tukio hilo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema wanajeshi hao waliokufa, 6 ni kutoka Malawi na 1 Tanzania.

”..Walinda amani wameuawa wakati wa operesheni ya pamoja iliyokuwa ikifanywa na Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa na Jeshi la Congo dhidi ya kundi LA Allied Democratic Foirces linalojulikana kama ADF.

”Taarifa za awali zinaonesha kuwa walinda amani wengine 10 wamejeruhiwa na mmoja hajulikani alipo”. Amesema Dujarric

Walinda amani kadhaa wa jeshi la Congo pia wameripotiwa kuuawa ama kujeruhiwa katika operesheni hiyo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya walinda amani waliouawa na serikali ya Jamhuri ya watu wa Malawi na ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Msemaji wa Umoja wa mataifa amesema pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameyasisistizia makundi yanayopigana kuacha kuacha mapigano, ambayo yanazidi kusababisha maafa kwa watu na pia ugumu katika kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo.

Wafanyakazi wa huduma za afya wanapata changamoto kuwapata na kuwahudumia wagonjwa walioambukizwa ugonjwa huo.

Mji wa Beni na vijiji vya jirani, umekuwa ukikabiliwa na mlipuko wa Ebola ambao umeshawaambukiza watu zaidi ya 300.

Mlipuko huu wa Ebola wa tatu kwa ubaya zaidi kuwahi kutokea baada ya ule uliotokea Afrika magharibi mwaka 2013 hadi 2016 ambako watu elfu 28 waliambukizwa na ule uliotokea Uganda mwaka 2000 ambako wagonjwa 425 waliripotiwa.

Makundi kadhaa ya wapiganaji likiwemo kundi la Ugandan Allied Democratic Forces, yanaendesha shughuli zake katika eneo hilo. Umoja wa Mataifa umeongeza hali ya tahadhari kutokana na kuendelea kwa mapigano katika eneo hilo na kuonya kuwa ghasia zinaweza kuzuia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini humo.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents