Habari

Wananchi Bulyanhulu wakosa imani na viongozi

WANANCHI waishio jirani na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu hawana imani na viongozi wa Serikali kwa walichokieleza kuwa asilimia kubwa ya viongozi wameshindwa kuwatetea na badala yake kuegemea upande wa wamiliki wa mgodi.

Na Zuhura Waziri, Kahama

 

WANANCHI waishio jirani na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu hawana imani na viongozi wa Serikali kwa walichokieleza kuwa asilimia kubwa ya viongozi wameshindwa kuwatetea na badala yake kuegemea upande wa wamiliki wa mgodi.

 

Wananchi hao walisema juzi kuwa asilimia kubwa ya viongozi wanachukua fedha kutoka kwa wamiliki wa mgodi na kushindwa kupeleka malalamiko yao sehemu husika ili waweze kutendewa haki.

 

Akitoa malalamiko hayo kwa Kamati ya Kuchunguza Mikataba ya Madini chini ya Mwenyekiti, Jaji Mark Bomani, kwenye mkutano wa hadhara, mmoja wa wananchi hao, Bw. Wiliam Mathias, alidai kuwa hawataki kusikia suala la kiongozi kusikiliza malalamiko zaidi ya Kamati hiyo.

 

Alisema mpaka sasa hawaoni kiongozi wa kumpelekea malalamiko yao kwa sababu wengi wanapochukua hushindwa kuyafikisha sehemu husika kwa sababu hupewa fedha ili wanyamaze.

 

“Yaani bora mmekuja na tuna imani kuwa haya yatafika, kwa sababu mmetumwa na Rais na mtetezi wetu, Zitto Kabwe yupo nanyi sivyo tusingekusanyika hapa, mngebaki mnaongea na miti, hakuna kiongozi hapa wilayani kwetu,” alisema Bw. Mathias.

 

Aidha, alisema siku chache zilizopita, mmiliki wa mgodi huo, aliandaa chakula na kuchinja ng’ombe ili kuwapoza machungu wasiseme yanayowakera kwa Kamati baada ya kuwahoji.

 

“Hawa watu wajanja sana wanajifanya wana akili mno kupita mtu yeyote yule, walivyosikia mnakuja, wakaandaa chakula na mang’ombe ili mkija tushindwe kusema, mchezo huo unatumika hadi kwa viongozi, wao wakija wanapewa bulungutu,” alisema.

 

Naye Bibi Sophia Bitageka, alidai mbele ya Kamati kuwa mmiliki wa mgodi huo na uongozi mzima, wamewadhulumu fedha zao ambazo walifanyia kazi ya kuchimba kokoto kwa miezi miwili iliyopita.

 

Alidai kuwa katika kijiji cha Bugarama, walipewa kazi ya kutwanga kokoto madebe mengi, lakini hadi sasa hawajalipwa na hawajui watalipwa na nani, kwa sababu mara wanapokwenda kumwona mhusika, huwaambia fedha alipewa Mtendaji wa Kijiji ambaye wakimfuata huwaambiwa hakuna fedha.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents