Habari

Wananchi wampinga mkuu wa wilaya Siha

WANANCHI wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wamepinga hatua ya mkuu wa wilaya hiyo kutangaza kuwa wamekubali kutoa eneo lao la mila ya jamii ya Kimasai kwa Chuo cha Polisi (CCP) mkoani hapa.

Na Magesa Magesa, Moshi


WANANCHI wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wamepinga hatua ya mkuu wa wilaya hiyo kutangaza kuwa wamekubali kutoa eneo lao la mila ya jamii ya Kimasai kwa Chuo cha Polisi (CCP) mkoani hapa.


Wananchi hao ni wa vijiji vya Orkolili, Ormelili na Embukoi ambao wamempinga mkuu huyo wa wilaya aliyedaiwa kutoa maelezo hayo mbele ya Waziri wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu juzi wakati akifunga mafunzo ya polisi chuoni hapo.


Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi wakiongozwa na wenyeviti wa vijiji hivyo, Bw. Lazaro Laitayo, Bw.James Lonyokie na Bw. Baraka Laizer , walisema hawajawahi kukaa na viongozi wa wilaya hiyo na kukubaliana kuhusu jambo hilo.


Walieleza kuwa mkuu huyo wa wilaya, alisema kuwa wananchi hao walikubaliana kutoa eneo la makazi na mila lenye ukubwa ekari 3,300 kwa chuo hicho cha mafunzo ya polisi jambo ambalo wao wamelipinga.


Wenyeviti hao walisema kauli ya mkuu wa wilaya inaonekana kutoa mwanya wa kuwanyanganya wananchi hao haki yao ya msingi kulingana na sheria na katiba ya nchi.


“Ni jambo la kusikitisha tumedhalilishwa. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haijafika hata kuona hali ilivyokuwa mbaya,tulivamiwa na askari Polisi tukavunjiwa nyumba zetu na tukaamriwa tuondoke, “alisema


Aidha walisema kuwa uongozi wa wilaya haujawahi kukutana nao na kuzungumzia suala hilo.


Walisisitiza kuwa eneo hilo ni la mila na linamilikiwa kisheria na jamii ya kabila la Kimasai kwa ajili ya matambiko na matukio makubwa ya jamii hiyo kutoka nchi za Afrika Mashariki.


“Tunapinga hadharani na tunaomba Ofisi ya Waziri Mkuu iangalie suala hili kwani inalifahamu wazi,”alisema Mwenyekiti wa Ormelili Bw. Laizer.


Viongozi hao walidai matamshi ya mkuu wa wilaya, yanapingana na ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro aliyewatembelea wananchi hao na kuahidi kumaliza mgogoro huo ifikapo Desemba mwaka huu.


Mkuu wa Wilaya ya Siha, Bi. Anna Rose Nyamubi alipoulizwa kwa njia ya simu na waandishi wa habari kuhusu suala hilo, alikataa kulizungumza na kuwaagiza kumwona Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi


Jitihada za kumpata mkuu wa chuo hicho, zilikwama baada ya simu yake kutopatikana hewani jana. Juhudi zaidi kumpata mkuu huyo kuzungumzia suala hilo, zinaendelea.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents