Habari

Wananchi wapambana na FFU

Zaidi ya wakazi 500 wa Wazo Hill eneo la Chasimba, jijini Dar es Salaam wakiwa wamebeba silaha za jadi, jana walipambana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakipinga kuondolewa katika eneo hilo.

Na Sharon Sauwa

 
Zaidi ya wakazi 500 wa Wazo Hill eneo la Chasimba, jijini Dar es Salaam wakiwa wamebeba silaha za jadi, jana walipambana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakipinga kuondolewa katika eneo hilo.

 

Tukio hilo lilitokea baada ya Mahakama ya Rufaa kulitupilia mbali ombi lao la kupinga kuondolewa katika eneo hilo, wakati wakisubiri kesi ya msingi kusikilizwa.

 

Nipashe lilifika katika eneo hilo na kukuta kundi kubwa la wakazi wa eneo hilo wakiwa na silaha za jadi, yakiwemo mapanga na mishale, huku chini kukiwa na mabaki ya maganda ya mabomu ya machozi yakiwa yamezagaa katika eneo hilo.

 

Mmoja wa viongozi wa wanaharakati wa eneo hilo, Bw. Aron Daniel, alisema baada ya uamuzi huo kutolewa, FFU walifika eneo hilo wakiwa na tingatinga na lori moja, yote yanayomilikiwa na Kiwanda cha Kutengeneza Saruji cha Wazo Hill.

 

Alisema baada ya kuingia katika eneo hilo, walipiga filimbi na wao walijitokeza kupinga kuondolewa katika eneo hilo.

 

`Walipotuona walianza kufyatua mabomu ya machozi,` alisema kiongozi huyo.

 

Alisema askari hao waliokuwa wamebeba bunduki na mabomu ya machozi walianza kutupa mabomu yao lakini wakazi waliosha nyuso zao kwa maji na kuendelea kubaki katika eneo hili,` alisema.

 

Alisema mabomu hayo yanasadikiwa kuwa kama 10 hivi, yalikwisha na askari hao waliwaambia wanakwenda kuongeza nguvu na kuahidi kuwa wangerudi baadaye.

 

Bw. Daniel alisema wataendelea kujikusanya katika makundi na kulinda nyumba zao zisibomolewe mpaka hapo serikali itakapoingilia kati mgogoro huo.

 

`Tuko tayari kupigwa risasi na kuuawa na askari lakini hatuwezi kuondoka katika maeneo haya kwa sababu hatuna maeneo mengine ya kwenda,` alisema kiongozi huyo huku akishangiliwa na wakazi hao.

 

Eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 990 linadaiwa kumilikiwa na kiwanda cha Wazo Hill huku wakazi hao wapatao 1000 nao wakidai kuwa ni wamiliki halali.

 

Hata hivyo, katika kesi hiyo watu 903 walijitokeza katika kufungua kesi mahakamani kupinga kuondolewa katika eneo hilo.

 

Kwa upande wake, wakili wa wakazi hao, Bw. Mabere Marando, alisema walipeleka barua ya kuiomba Mahakama ya Rufaa kusitisha amri ya kuondolewa katika eneo hilo mpaka hapo kesi yao ya msingi itakaposikilizwa.

 

Alisema mahakama hiyo chini ya Jaji Munuo, jana ilikataa ombi hilo na kutaka wakazi hao wabomoe nyumba zao.

 

`Uamuzi uliotolewa leo (jana) ni wakazi hao waondoke katika eneo hilo na kama wakishinda katika kesi ya msingi basi watalipwa fidia nyumba zao,` alisema Bw. Marando.

 

Wakili huyo alisema wakazi hao wameamua kukata rufaa tena kuhusiana na uamuzi huo na kwamba alikuwa akishughulikia suala hilo jana.

 

Hata hivyo, alisema kwenda kuwaondoa katika eneo hilo kwa siku ya jana ni kinyume cha sheria.

 

Bw. Marando alisema sheria inawataka mara baada ya kushinda kesi hiyo, warudi tena Mahakama Kuu kwa ajili ya kuomba kibali cha amri ya kuwaondoa katika eneo hilo.

 

Alisema sheria inasema baada ya uamuzi huo, wakazi hao wanatakiwa kuhama eneo hilo ndani ya siku 14.

 

Naye Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Alfred Tibaigana, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema kuwa FFU walikuwa katika doria ya kawaida.

 

`Hatuwezi kuwataka waondoke wakati leo hii (jana), uamuzi umetolewa na kuna utaratibu wa kufanya kabla ya kuwaondoa,` alisema.

 

Alisema baada ya maamuzi ya mahakama, wananchi hao waliamua kwenda kufunga njia na kuchimba mashimo katika barabara za eneo hilo.

 

Wakati tunakwenda mitamboni, kulikuwa na taarifa ambazo hazikuthibitishwa kwamba FFU walirejea eneo hilo na kutupa tena mabomu ya machozi.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents