Habari

Wanandoa wafa ajalini Dar

WANANDOA wamefariki dunia jijini Dar es Salaam, baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Mandela, eneo la Mabibo Relini.

NA MAGRETH KINABO


WANANDOA wamefariki dunia jijini Dar es Salaam, baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Mandela, eneo la Mabibo Relini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow, alisema wanandoa hao walifariki dunia juzi usiku, baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili STJ 8446, aina ya Toyota Land Cruiser mali ya serikali.
Alisema ajali hiyo ilitokea saa 5:00 usiku, wakati gari hilo lililokuwa likitokea Ubungo kwenda Buguruni, lilipowagonga wanandoa hao waliokuwa wakipita njia.
Kamanda Rwambow aliwataja wanandoa hao kuwa Christian Haule (60), ambaye ni mfanyabiashara ndogo ndogo na mkazi wa Mabibo CCM, aliyefariki dunia papo hapo, wakati mkewe, Joyce Ngairo (50), aliyekuwa mama wa nyumbani, alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitali ya Amana, kwa ajili ya kupata matibabu.
Alisema dereva aliyesababisha ajali hiyo hajapatikana kwa kuwa alikimbia, baada ya tukio hilo.
Kamanda Rwambow alisema maiti zimehifadhiwa katika hospitali ya Amana. Polisi wanamtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwa marehemu, mmoja wa wanafamilia, Joseph Ndauka alisema wanandoa hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakirejea nyumbani wakitoka kwenye shughuli ya komunio eneo la Tabata Kimanga.
Ndauka alisema mazishi yatafanywa kwa pamoja keshokutwa katika makaburi ya Mabibo, baada ya watoto wa marehemu kuwasili kutoka Songea.
Alisema wanandoa hao wameacha watoto na wajukuu kadhaa, wakiwemo wawili waliokuwa wakiishi nao.
Haule pia amemuacha mama yake mzazi mwenye umri wa zaidi ya miaka 80, aliyekuwa akiishi naye nyumbani kwake Mabibo.


Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents