Wanandoa wapigwa mawe hadi kufa

Wanandoa wameuawa kikatili kwa kupigwa mawe na kuchapwa viboko hadi kufa huku wakiwa wamefungwa kamba na wananchi wilayani Karagwe mkoani Kagera

Na Kibuka Prudence, PST Kagera

Wanandoa wameuawa kikatili kwa kupigwa mawe na kuchapwa viboko hadi kufa huku wakiwa wamefungwa kamba na wananchi wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Bw. George Mayunga, alisema mauaji hayo yalitokea katika kijiji cha Lutunguru kitongoji cha Kilela, saa saba mchana ambapo wanandoa hao walivamiwa na kupigwa mawe na kikundi cha wananchi hao.

Bw. Mayunga, aliwataja marehemu hao kuwa ni Bw. Koronely Mboyerwa (69) na mke wake, Bi. Josephina Kolonery (56).

Alisema kabla ya mauaji hayo ya kikatili, kundi hilo lilifika nyumbani kwa Bw. Mbeyerwa na kuwafunga kamba na kuanza kufyeka shamba la migomba na kubomoa nyumba yao upande mmoja na kisha kuchoma vitu mbalimbali kama magodoro na vyakula.

Baadaye wananchi hao waliwachukua na kuwapeleka eneo la Kilela katika barabara ya Kaisho kwenda Mulongo na kuanza kuwashambulia kwa mawe na kuwapiga kwa fimbo hadi walipofariki dunia.

Kamanda aliiambia PST kuwa hadi sasa watu saba wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Kuraish Rwabitenga (36), Jumanne Cyprian (25), Focus Barnabas (48), ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji Rugalama, Theobard Thomas (45) na Augustino Batromeho (46).

Wengine ni John Simon (33), ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji Omumabale na Renatus Selestine (31), wote wakazi wa Kaisho wilayani Karagwe.

Bw. Mayunga alisema chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na jeshi la polisi linaendelea na upelelezi wa tukio hilo.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents