Siasa

Wanaoambukiza ukimwi siku zahesabika-Kikwete

Rais Jakaya Kikwete, amesema watu wote wanaojijua kuwa wameathirika na Ukimwi na kuwasambazia wengine kwa makusudi siku zao zinahesabika.

Na Jackson Kalindimya, Tabora


Rais Jakaya Kikwete, amesema watu wote wanaojijua kuwa wameathirika na Ukimwi na kuwasambazia wengine kwa makusudi siku zao zinahesabika.


Rais Kikwete pia ametangaza hadharani majibu ya vipimo vyake vya VVU kuwa yanaonyesha hajaathirika.


Amesema kuna watu wanajijua kuwa wanaishi na VVU lakini wamekuwa wakitumia vishawishi au njia nyingine zozote zile, kuwaambukiza wengine.


Akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, yaliyofanyika mjini hapa kitaifa jana, Rais Kikwete alisema sheria mpya ya Ukimwi itakapopitishwa na Bunge Februari mwakani, itawabana watu hao na kuwalinda watu wasiambukizwe Ukimwi kwa nguvu na watu wanaojijua kuwa wameathirika.


“Mtu huyo akitajwa kuwa ni mwathirika wa Ukimwi na anatumia hila mbalimbali zikiwemo fedha, mali au njia nyingine kuwaambukiza watu wengine atakamatwa na kupimwa kisha akibainika kuwa�anao�sheria itachukua mkondo wake“, alisisitiza.


Rais Kikwete alisema, licha ya sheria hiyo kuwabana watu hao, pia watu wote wanaowanyanyapaa na kuwatenga watu wenye virusi vya Ukimwi, ikiwa pamoja na kuwanyima haki zao za msingi nao hawatavumiliwa.


Akizungumzia mkakati wa upimaji kwa hiari, alisema anapenda kuona Tanzania inasifika kwa uhodari wa kuzuia watu wapya wasiambukizwe zaidi, badala ya uhodari tu wa kuwahudumia watu walioambukizwa Ukimwi.


�Rais Kikwete alisema taifa linajiandaa kuwahudumia waathirika wa Ukimwi na kati ya watu 220,000 waliothibitika kuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi, kati yao 120,000 tayari wanahudumiwa na waliobaki taratibu za kuwahudumia zinakamilishwa.


“Tunataka waathirika wa Ukimwi wahudumiwe ili waweze kuishi maisha ya kawaida na kusogeza siku zao za kuishi“ aliuambia umati uliojitokeza kuhudhuria maadhimisho hayo.


Rais akigusia changamoto ya kupokea majibu baada ya kupima, alisema kuwa, wakati alipopima Ukimwi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, kuzindua kampeni ya upimaji kwa hiari, alikuwa na changamoto kubwa ya kuyasubiri majibu yake, lakini kwa kuwa anajiamini, anashukuru Mungu kuwa majibu yalionyesha kuwa yuko salama.


“Nilikuwa chumbani na Profesa Mwakyusa, ambaye yawezekana alikuwa na hofu kubwa zaidi kuhusu majibu ya Rais, yakiwa mabaya itakuwaje?�lakini majibu yakatoka ni salama.


Nawahimiza wananchi wote wakabili changamoto za kupima na kupokea majibu“ aliasa.


Kuhusu mwenendo wa zoezi la upimaji kwa hiari, alisema kuwa, zoezi hilo linakwenda vizuri na analifuatilia kwa karibu sana ili kuhakikisha kuwa linatoa matokeo yanayotarajiwa kwa manufaa ya taifa.


“Changamoto kubwa ni upya au ugeni wa zoezi hili. Kuna hofu na changamoto mbalimbali zikiwemo za walengwa, usafirishaji wa vifaa vya kupimia na posho za wapimaji ambazo zinashughulikiwa “ alisema.


Kikwete pia alisema serikali imeweka mipango endelevu ya miaka mitano 2008- 2012 kupambana na ukimwi, ikiwa pamoja na kuboresha huduma za uzuiaji na�upimaji, kinga na tiba.


Alisisitiza kuwa hali ya maambukizi bado ni ya kutisha na kwamba kila mmoja� ana wajibu wa�kutilia mkazo� jitihada kubwa za kuzuia ongezeko la wanaoathirika na� jamii kushirikiana na serikali katika uzuiaji maambukizi mapya kwa kuwa waaminifu katika mahusiano na kutumia kinga wanapofanya tendo la ndoa.


Aliwaonya pia watu wanaofuja mali zinazolengwa kwa waathirika wa Ukimwi na kujinufaisha wao kuwa hawatavumiliwa.


Waziri wa Afya, rofesa David Mwakyusa, akizungumza katika maadhimisho hayo ambayo kauli mbiu yake ni `Zuia Ukimwi,Timiza wajibu wako na Ongoza Mapambano`, alisema matokeo ya awali ya upimaji Ukimwi nchini, yanaonyesha kuwa watu milioni 2.5 sawa na asilimia 60.1 tayari wamepima. Lengo ni watu milioni 4.1 katika kipindi cha miezi sita tangu kuanza kwa zoezi hilo.


Aliitaja mikoa inayofanya vizuri zaidi kuwa ni Lindi iliyofikisha asilimia 115 na Kilimanjaro asilimia 96. Tabora ni ya 17 ambayo imefikisha asilimia 43.4. Wanawake ndio wanaoongoza kwa kujitokeza kupima.


Aliitaka mikoa yote kuendelea na upimaji wa hiari hata baada ya kupita kwa kipindi hicho, kwani zoezi la upimaji ni la kudumu na kuwataka wanaume nao kujitokeza kwa wingi kupima ili kujua hali ya afya zao.


Balozi wa Marekani nchini, Mark Green alimpongeza Rais Kikwete kwa namna alivyojitokeza kuongoza upimaji kwa hiari na kuwa mfano wa kuigwa.


Alisema binadamu sasa wanaishi katika kipindi cha misukosuko mikubwa katika historia ya maisha ya mwanadamu.


Balozi Green alisema katika nyakati zijazo,watoto na wajukuu zetu watapenda kujua kitu gani alichokifanya kila mmoja wetu katika vita dhidi ya Ukimwi na kujitoa kiasi gani katika kudhibiti maambukizi hayo.


Miongoni mwa waliohudhuria maadhimisho hayo ni Spika wa Bunge, Samwel Sitta, Waziri anayeshughulikia masuala ya Bunge, Dk. Batilda Buriani, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Abeid Mwinyimusa, Mwenyekiti wa TACAIDS, Dk. Fatuma Mrisho na viongozi wengine.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents