Wanaochanganya Dizeli na Mafuta ya taa Wabainika

Wananchi wanaotumia mafuta aina ya dizeli wanatakiwa kuwa makini kwani hivi karibuni imebainika kuwa vituo vingi vya mafuta vinauza dizeli iliyochanganywa na mafuta ya taa kwa lengo la kupata faida zaidi.

Wananchi wanaotumia mafuta aina ya dizeli wanatakiwa kuwa makini kwani hivi karibuni imebainika kuwa vituo vingi vya mafuta vinauza dizeli iliyochanganywa na mafuta ya taa kwa lengo la kupata faida zaidi.

Maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) wamethibitisha kuwa uchanganyaji huo ambao unajulikana kama ‘kuchakachua’ unaendelea kufanywa licha ya kutambua kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria na pia unaweza kusababisha athari kubwa sana kwenye vyombo vinavyotumia bidhaa hiyo.

Anayekaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alitoa mfano kuwa kati ya sampuli 221 zilizochukuliwa na mamlaka yake kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi mwezi uliopita iligundulika kuwa sampuli 128 mafuta yake yalikuwa yamechanganywa.

“Tatizo ni kubwa licha ya kuwa tunapambana nao, lakini hali halisi ndiyo ilivyo,” alisema Samwel alipozungumza juzi kwenye warsha ya wahariri iliyofanyika mjini Bagamoyo. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebo alisema tatizo la uchanganyaji wa mafuta linafanywa kutokana na wafanyabiashara kutaka kupata faida zaidi kutokana na mafuta ya taa kodi yake kuwa ndogo kuliko ya dizeli.

“Serikali iliamua kuweka kodi ndogo kwenye mafuta ya taa kwa kutambua kuwa wananchi wengi wa vijijini wanayatumia hivyo uamuzi huo ulikuwa ni wa kumsaidia mwananchi wa kawaida,” alisema Masebo.

Mkurugenzi huyo alisema kutokana na kodi ndogo ya mafuta taa wafanyabiashara wanatumia mwanya huo kuyachanganya na dizeli hali aliyodai inamwathiri mteja.

Katika kupambana na tatizo hilo mamlaka yake kwa sasa ina mpango wa kuweka rangi (fuel mark) kwenye mafuta kung’amua mafuta yaliyochanganywa, alisema.

Alisema mpango mwingine ni kuanzisha maabara zinazotembea (Mobile Laboratory) kuwezesha kupima sampuli za mafuta kwenye vituo na kutoa majibu papo kwa hapo.

Alisema kwa sasa mamlaka yake inashindwa kuchukua hatua za haraka kwa vile vipimo kwa sampuli moja vinaweza kuchukua siku tatu na kama itagundulika mafuta yamechanganywa wateja wengi watakuwa wamekwisha kuathirika. “Hili la vipimo kuchukua siku tatu siyo zuri.

Tunataka tuwe na maabara kwenye vituo tukichukua sampuli na kutoa matokeo hapo hapo,” alisema Masebo.

Hatua nyingine ambayo Mkurugenzi huyo aliitaja ni kuiandikia Wizara ya Nishati na Madini kuangalia kodi kwenye mafuta na ikiwezekana kodi zote ziwe sawa kuondoa tatizo hilo. Alisema iwapo kodi ya mafuta ya taa itakuwa sawa na dizeli anaamini kuwa tatizo hilo litapungua kama siyo kuondoka kabisa.

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents