`Wanaoua` maalbino wanaswa

Wakati watu 172 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji kutokana na imani za kishirikina, hususani albino, wakiwemo waganga wa jadi 71 wametiwa mbaroni

Na George Ramadhan, PST Mwanza


Wakati watu 172 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji kutokana na imani za kishirikina, hususani albino, wakiwemo waganga wa jadi 71 wametiwa mbaroni, mtoto ambaye ni albino amenyimwa nafasi ya kusoma katika shule moja Kibaha kutokana na ulemavu wake.

Kuhusu waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Bw. Zelothe Stephen alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni maalum inayolenga kukomesha mauaji ya albino na vikongwe.

Kwa mujibu wa Kamanda Stephen, operesheni hiyo ilifanyika baada ya kumalizika kwa kongamano la kujadili mauaji ya albino na vikongwe na kutafuta njia za kukomesha mauaji hayo.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na ushirikiano wa wananchi, viongozi na waganga wa tiba asili ambao hawajihusishi na upigaji ramli.

Aliwataka wananchi pamoja na wadau wengine, kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua waganga wanaopiga ramli pamoja na wanaotekeleza mauaji hayo ili kukomesha mauaji ambayo yamewafanya albino sasa kuishi kwa wasiwasi mkubwa.

Hata hivyo, Kamanda hakutaja majina ya watuhimiwa kwa maelezo kwamba bado uchunguzi unaendelea.

Habari za kukamatwa kwa watuhumiwa hao katika eneo hili la Kanda ya Ziwa ambako ndiko tatizo la mauaji ya albino na vikongwe ni kubwa, linaweza kusaidia kupunguza kasi ya mauaji na kuwafanya sasa watu wenye ulemavu huo kupumua angalau kidogo.

Kwa kipindi kirefu, toka wimbi la mauaji ya albino lilipuke nchini, wanajamii wakiwemo maalbino wenyewe, wamekuwa wakilalamikia serikali kwa madai kwamba hawaoni kama hatua zinazotia matumaini zinachukuliwa.

Wakati huo huo, Edwin Agola anaripoti kutoka mkoani Pwani kwamba mwanafunzi Salehe Omary, amekataliwa kupewa haki ya kusoma katika Shule ya Msingi Mkuza mkoani Pwani, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni albino.

Mwanafunzi huyo mwenye miaka tisa alikataliwa kuanza darasa la kwanza shuleni hapo mwaka jana baada ya uongozi wa shule kudai kuwa hakuna huduma kwa ajili ya walemavu hao.

Hata hivyo, mwanafunzi huyo baada ya kukataliwa kusoma, wanaharakati za kutetea haki za albino mkoani Pwani walihaha hadi wakafanikiwa kumsajili katika Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam na sasa anaendelea na masomo ya darasa la kwanza.

Mwalimu wa darasa la kwanza wa Mkuza, Bi. S. Twalib, alidaiwa ‘kumtimua’ mwanafunzi huyo akisingizia ukosefu wa vifaa maalumu kwa ajili ya mafunzo ya alibino.

Alipofuatwa na Nipashe, Bi. Twalib alisema mtoto Salehe ana matatizo ya kuona na alihitaji miwani, hivyo ilikuwa vigumu kumuendeleza kwani alishindwa kuandika kwa ufasaha.

Sababu zilizotolewa na wakosoaji zilipinga maelezo hayo wakisema huko ni kuwanyanyasa walemavu na kwamba hakuna shule inayotoa vifaa kwa ajili ya albino.

Mwalimu Mkuu wa Uhuru Mchanganyiko, Bw. Ditrick Mkwera, akizungumzia juu ya mtoto huyo aliyeandikishwa mwaka huu, alisema Salehe anafanya vizuri darasani na anafundishika.

“Tulichofanya nikumuweka kwenye viti vya mbele ili aone ubaoni na walimu kumfuatilia kwa karibu. Hivi ndivyo maalbino wanafanywa katika mashule yote… Kwakweli anajitahidi ni mwanafunzi mwenye kiu ya elimu,“ aliongeza.

Shirika la kiraia la kutetea haki na maendeleo ya walemavu (ADD) lilitoa taarifa za mtoto huyo kakataliwa masomo kwa sababu ya maumbile yake.

Akizungumzia suala hilo, bibi wa Salehe, Bi. Tisa Omary, alisema baada ya kukataliwa kusoma pale Mkuza mtoto huyo alianza kuzurura na kukata tamaa.

Aliwashukuru ADD kwa kuibua tukio hilo na kuutaka umma kuwasaidia albino kwa kuwa si ugonjwa bali ni hali ya kimaumbile.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents