Habari

Wanaouza wasichana nchi za nje kusakwa

Serikali imetangaza kuwasaka kwa udi na uvumba watu wanaojihusisha na biashara ya kuwauza wasichana wa Kitanzania nje ya nchi.

Na Simon Mhina



Serikali imetangaza kuwasaka kwa udi na uvumba watu wanaojihusisha na biashara ya kuwauza wasichana wa Kitanzania nje ya nchi.


Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto Bi. Sophia Simba amesema serikali imeamua kuwasaka kwa udi na uvumba watu wanaofanya biashara ya kuuza wasichana wa kitanzania kwenda nchi za nje, ili kuepuka aibu inayoikabili.


Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Waziri huyo alisema awali mtindo huo mchafu ulikuwa umeshamiri nchini kati ya mkoa na mkoa, lakini sasa ni jambo la kusikitisha kusikia kwamba biashara hiyo haramu imevuka mipaka.


Mhe Simba alisema amesikitika mno baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba kuna maajenti huwachukua wasichana wadogo kutoka mikoa na miji ya mipakani na kuwaleta jijini Dar es Salaam na kuwasafirisha hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


“Kwa kweli biashara hii imetusikitisha na kutuudhi sana, Huu sio tu ni ukatili dhidi ya binadamu, lakini kubwa zaidi ni aibu ambayo Tanzania tunaweza kupata, yaani badala ya kusafirisha bidhaa nchi za nje, wenzetu wanasafirisha binadamu?


Huu ni ukatili wa hali ya juu tena ni aibu kubwa,“alisema waziri huyo.


Alisema taarifa hizo zimekuja wakati wa maadhimisho ya wiki ya kupiga vita dhidi ya ukatili wa kijinsia.


Alisema kutokana na tatizo hilo kuvuka mipaka, wizara yake itashirikiana na vyombo vyote vya dola katika kuwasaka wahusika, na kulitatua tatizo hilo mara moja.


Hata hivyo, Waziri Simba alisema ili kutafuta chanzo cha mizizi ya tatizo hilo, wizara yake itafuatilia kwa karibu kwa wazazi wanaowatoa watoto wao, ili kujua sababu ya kufanya hivyo.


“Tunajua wengi huchukuliwa kwa madai kwamba wanakwenda kutafutiwa kazi za ndani mijini au vibarua, sisi kupitia kwa maafisa ustawi wa jamii tutafuatilia kwa wahusika ili tujue hao wanaowachukua ni kina nani na wanawapeleka wapi,“alisema.


Waziri huyo aliwaomba wananchi wema kushirikiana na wizara yake, kutoa taarifa sehemu yoyote ambayo wanaona kuna mkusanyiko usio wa kawaida ambao unajumuisha wasichana wadogo.


Alisema wizara yake itashirikiana na polisi jamii, katika kupokea taarifa kama hizo ili kukomesha biashara hizo, na kuliondolea aibu taifa.


Katika kukomesha biashara hiyo, Waziri Simba aliwataka wazazi kuwa macho kwa watu wanaokwenda mikoani na kudai kwamba wanatafuta watoto wa kazi.


“Hili ni kosa linalofanana na utekaji kabisa, unajua mtoto hana anachokijua, hana maamuzi yoyote zaidi ya kutegemea maagizo toka kwa mlezi au mzazi, sasa Baba au mama anapomruhusu aambatane na mtu yoyote, mtoto huwa anamwamini mtu huyo asilimia mia moja, ndio maana wanajikuta wanaingizwa katika mdomo wa mamba na watu hao, kwa vile lengo lao la kuwatoa mikoani kuwaleta mijini, halikuwa jema,“alisema na kuongeza “ninawaomba watanzania tushirikiane tuwalinde watoto wetu dhidi ya ukatili huu“


Aliwaomba wazazi wawe mstari wa mbele katika kutoa taarifa za watu wanaofanya ukatili huo.


Pia aliwaomba kuacha tamaa ya fedha na kupuuza ahadi zinazotolewa na watu hao.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents