Michezo

Wanariadha wa Tanzania kuanza kibarua kesho London

Timu ya Taifa ya Riadha inayoshiriki mashindano ya Dunia ya riadha yanayoendelea jijini London inatarajia kuanza kibarua chake cha kuipeperusha bendera ya  Tanzania hapo kesho siku ya Jumamosi ambapo mfukuza upepo,  Failuna Abdi Matanga atakimbia mbio za mita 10,000 leo huku akishuhudiwa na  maelfu ya watanzania kupitia DStv Muda wa saa mbili usiku.

 Balozi maalum wa DStv Alphonce Simbu (Kushoto) akiwa na Wanariadha wenzake Nelson Mbuya (wa pili kushoto), Stephano Huche na Joseph Panga(kulia) wakiwa katika mazoezi makali hivi karibuni

Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania,  Maharage Chande amesema DStv imefanya jitihada kubwa na kuhakikisha kuwa watanzania wanaishuhudia timu yetu ikituwakilisha katika mashindano hayo muhimu ulimwenguni.

“Tunawahakikishia watanzania burudani hii moja kwa moja kupitia DStv chaneli za Supersport. Tunaamini sote tutakuwa nyuma yao wachezaji wetu kuwashuhudia jinsi wanavyotuwakilisha” alisema Maharage

“Suala la watanzania kuwashuhudia vijana wetu wakishiriki katika mashindano makubwa kama haya lina maana kubwa sana. Vijana wadogo wakiwaona dada zao na kaka zao wakishiriki mashindano makubwa kama haya inawatia moyo na kuwapa ari na tamaa ya wao kujitahidi na kufika hatua kama hizo. Hili ni jambo la muhimu sana na sisi DStv tunalitilia mkazo sana. Ni njia moja wapo ya kuwashawishi na kuwatia moyo vijana wetu wanaochipukia na kuwajengea kujiamini”

Baada ya Failuna anayekimbia mita 10,000, watanzania watashuhudia tena shughuli pevu siku ya jumapili kuanzia majira ya saa nne asubuhi ambapo washiriki watatu – Alphonce Felix Simbu, Ezekiel Jafari Ng’imba na Stefano Huche Gwandu watakuwa wakikata upepo katika viunga vya jiji la Malkia London ikiwa ni mbio ndefu za kilomita 42.

Wakati wawakilishi wakike wao wataingia barabarani ambapo Tanzania inawakilishwa na Sara Ramadhani Makera na Magdalena Crispin Shauri ambao nao watafukuza upepo umbali wa kilomita 42 majira ya saa nane mchana.

Wanariadha wawili wa mbio fupi za mita 5,000, Emmanuel Giniki Gisamoda na Gabriel Gerald Geay wanatarajia kukimbia katika mashindano hayo siku ya Jumatano tarehe 9 Agosti majira ya mbili usiku hii ikiwa ni raundi ya mchujo na wakifuzu watashiriki fainali ya mita 5,000 siku ya Jumamosi tarehe 12 Agost majira ya mbili usiku.

Mashindano ya Dunia ya Riadha yalianza rasmi 1983 ambapo Tanzania imewahi kupata medali 1 tu ya Fedha kupitia mwanariadha Christopher Isegwe kwenye mbio za Marathon mwaka 2005 Helsinki Finland.

London Marathoni ni mashindano ya pili kwa ukubwa baada ya Olimpiki ambapo nchi 204 zinashiriki mashindano hayo mwaka huu. Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo ni kwa mara ya kwanza Tanzania imepeleka vijana wengi ambapo mwaka huu inawakilishwa na wanariadha 8.

Wanariadha wote wanaoshiriki wamefikia viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

By Hamza Fumo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents