Habari

Wanasiasa Kenya wadaiwa kusaka nguvu za giza nchini

Imedaiwa kuwa baadhi ya wanasiasa wanaowania nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao Kenya, wameanza kuwasili nchini kusaka nguvu za waganga wa kienyeji ili washinde katika kinyang’anyiro hicho.

Wanasiasa hao wanaripotiwa kumiminika katika miji ya Tarime, Musoma na Mwanza ambako hukutana na waganga ili kukamilishiwa mipango ya kushinda uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu.

Taarifa zilizonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya zinasema waganga hao wamekuwa wakiwapa wanasiasa hirizi ili kuwapoka wapinzani wao wapigakura.

Gazeti la Taifa Leo limeripoti kuwa, wengi wa wanasiasa hao walianza kumiminika nchini Februari, kabla ya mchujo kufanyika.”Wengi wa wagombea wanaamini hawawezi kupata ushindi bila usaidizi wa nguvu za kishetani.

Tumekuwa tukiwaona wengi wao wakipitia hapa na kuingia Tanzania,” alisema mkazi aliyejitambulisha George Ogwang alipozungumza na gazeti la Taifa Leo.”

“Ninamfahamu mmoja wa wanasiasa aliyepokea huduma za waganga hao na bado akabwagwa kwenye mchujo,” alisema.

Kwa miaka mingi wanasiasa katika eneo la Afrika Mashariki wamekuwa wakihusishwa na waganga wa kienyeji wanapoanza mchakato wa kusaka kura wakati wa uchaguzi.

Hivi karibuni, mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’ alizua gumzo bungeni aliposema ni wabunge wawili au watatu tu ambao ndio hawakupita kwa waganga wa kienyeji wakati wa uchaguzi uliopita.

Chanzo: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents