Habari

Wapangaji wa NHC wapinga kodi mpya

WAPANGAJI wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wamesema mpango wa shirika hilo kupandisha kodi ya pango kutoka Sh19,500 hadi 56,500 ni njama za kuwaondoa wapangaji wasio na uwezo katika nyumba hizo ili kuwapangisha wapangaji wengine wenye uwezo.



Na John Stephen


WAPANGAJI wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wamesema mpango wa shirika hilo kupandisha kodi ya pango kutoka Sh19,500 hadi 56,500 ni njama za kuwaondoa wapangaji wasio na uwezo katika nyumba hizo ili kuwapangisha wapangaji wengine wenye uwezo.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Kamati ya Kutetea Haki za Wapangaji wa Shirika hilo, Nyengi Ngawao, alisema kiasi hicho ni kikubwa na kwamba hawataweza kukilipa kwani wengi wa wapangaji hao ni wastaafu na wajane.


Ngwao alisema ongezeko hilo, litawaondoa katika nyumba hizo kwa kuwa sheria mpya inasema endapo mpangaji atashindwa kulipa kodi ya pango, atapaswa kuondoka.


Ngwao alisema tayari kesi namba 52/2007 imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Nyumba, kupinga ongezeko hilo na kwamba shirika hilo halikuwashirikisha kabla ya kutangaza kodi hiyo ambayo ilitangazwa rasmi mwanzoni mwa mwezi huu.


“Hatukubaliani na maamuzi ya upande mmoja licha ya awali serikali kusema kuwa tushirikishwe katika suala la kupanga kodi mpya. Kushirikishwa ni haki yetu ya kikatiba lakini uongozi wa NHC walitupuuza,” alisema Ngawao.


Alisema mbali ya kufungua kesi, tayari wamewasiliana na uongozi wa NHC Ilala kulalamikia ongezeko hilo pamoja na kutoshirikishwa katika kupanga ongezeko la kodi hiyo.


Msemaji huyo aliwataka wapangaji wa shirika hilo nchi nzima kuiunga mkono kamati hiyo, ili kuwa na msimamo mmoja katika kupinga ongezeko hilo na kwamba, wanapaswa kuendelea kulipa kodi ya zamani hadi mahakama itakapotoa uamuzi kuhusiana na madai yao.


” Tayari mahakama imetoa amri kwa NHC ili wasitoze kodi mpya, hivyo nawaomba wapangaji waendelee kulipa kodi ya zamani,” alisema msemaji huyo.


Shirika hilo lilisema limeongeza kodi hiyo ili liweze kukarabati nyumba hizo na kwamba kodi zinazotozwa sasa haziendani na hali halisi ya sasa.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents