Habari

Wapendekeza Rais Mugabe aongoze hadi kifo kimkute madarakani

Umoja wa Vijana wa chama cha Zanu PF nchini Zimbabwe umeomba Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe aruhusiwe kuongoza nchi hiyo hadi atakapokutwa na umauti.

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Mapendekezo hayo yamekuja katika wakati huu ambapo wanachama wengi katika chama hicho tawala kwenye majimbo nchi nzima walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita na kuamua kuitisha mkutano wa dharura mwezi Desemba kuzungumzia sakata la Mugabe kushindwa kumuandaa mrithi wake kwa miaka 37 aliyokaa madarakani.

Kwa mujibu wa gazeti la NEWS24 taarifa zimeeleza kuwa vijana hao wamefikia maamuzi hayo ya kuwasilisha maombi hayo baada ya taarifa kutoka kwenye kamati ya nidhamu ya Chama hicho kuwasilisha jina moja la mrithi wake ambapo ametajwa kuwa ni mke wa Rais Mugabe, Grace Mugabe.

Kwa kile kinachoonekana ni mpasuko ndani ya Chama cha Zanu PF, tayari Waziri wa Ulinzi nchini humo, Emmerson Mnangagwa ameunda kundi ndani ya chama hicho liitwalo ‘Team Lacoste’ linalompigia upatu kuongoza taifa hilo kama mrithi wa Mugabe.

Kwa upande mwingine Bi. Grace Mugabe yeye anaungwa mkono na kundi la vijana lijulikanalo kwa jina la ‘Generation 40’ huku likimpiga vita Bwana Mnangagwa kugombea nafasi hiyo ya urais.

Hata hivyo, tayari mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Zanu PF, Mubuso Chinguno amesema chama hakina mgombea mwingine zaidi ya mzee Mugabe (93) licha ya kuwa umri wake umemtupa mkono.

Mugabe ni Rais wetu wa maisha, hatuna tatizo nae hata akifia ofisini kwa hiyo tunakaribisha mapendekezo haya mapya ya kuwepo kwa kongamano kujadili hilo na baadae kuwasilisha kwenye mkutano mkubwa wa mwaka mwezi Desemba mwaka huu.” amesema Mubuso Chinguno kwenye mahojiano yake na gazeti la NEWS24.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents