Habari

Wapiga debe 140 wakamatwa Dar

Police Jijini Dar es Salaam inawashikilia zaidi ya wapiga debe 140 waliokiuka agizo la Mkuu wa Mkoa Bw. Abbas Kandoro la kuwataka ifikapo Julai Mosi kutoonekana katika vituo vya mabasi.

Na Grace Chilongola, PST



Police Jijini Dar es Salaam inawashikilia zaidi ya wapiga debe 140 waliokiuka agizo la Mkuu wa Mkoa Bw. Abbas Kandoro la kuwataka ifikapo Julai Mosi kutoonekana katika vituo vya mabasi.


Kati ya wapiga debe hao, 49 wamefikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka ya kusababisha usumbufu kwa abiria.


Miongoni mwa wapiga debe hao ni wale waliokuwa stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya Ubungo waliokuwa wakiwabugudhi baadhi ya abiria waliokuwa wakienda katika stendi hiyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo za safari.


Agizo hilo lilitolewa Juni mwaka huu na Bw. Kandoro ambapo aliwapa wiki mbili za kujitafutia kazi nyingine halali tofauti na hiyo ya kupiga debe katika vituo vya mabasi.


Akizungumza na Nipashe jana, Kaimu Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Liberatus Barlow, alisema katika msako unaoendelea kufanyika kwenye vituo vya mabasi umefanikiwa kuwakamata wapiga debe hao wakiwa wanaendelea na kazi hiyo ambayo Mkuu wa mkoa alishawaonya kuonekana katika vituo hivyo.


Alisema katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni polisi ilifanikiwa kuwakamata wapiga debe 19 katika baadhi ya vituo vya mabasi.


Kamanda Barlow alisema katika mkoa wa kipolisi wa Ilala polisi inawashikilia wapiga debe 44.


Alisema kwa upande wa mkoa wa kipolisi wa Temeke polisi kutoka siku ya kwanza ya zoezi hilo lilipoanza hadi kufikia juzi jumla ya wapiga debe 62 wameweza kukamatwa.


Alisema wapiga debe hao walikamatwa katika vituo tofauti vya mkoa huo.


Wakati huo huo, wapigadebe 29 wa jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika mahakama ya Jiji kwa tuhuma za kusababisha usumbufu kwa abiria.


Watuhumiwa hao wamepelekwa rumande baada ya kushindwa dhamana ya sh. 100,000 kila mmoja.


Waliofikishwa mahakamani hapo ni Salum Mohamed (17), Zuberi Rashid (22), Juma Ngumbuli (17), Fadhili Hamisi (22), Ally Said (26), Fikiri said (25), Abdallah Salehe (25), Ibrahim Ramadhan (22), Jofrey James (22) na Josephat Kazimoto (20).


Wengine ni Mbwana Ramadhan (20), Said Mshamu (27), Mateso Mapigi (25), Said Ally (25), Sumari Omdi (20), Mohamed Hemedi (17), Joshua Nsasu (19), Ramadhan Mohamed (30) na Idrisa Seleman (18).


Watuhumiwa wengine ni Shukuru Mohamed (24), Senga Ramadhan (28), Hamis Abdallah (37), Marick Bedson (22), Shaban Sultan (20), Juma Mgunda (28), Fadhil Mohamed (29), Hassan Ally (20), Miraji Maulid (25) na Salum Omary (30).


Ilidaiwa mahakamani na Grayson Fue, kuwa, wapigadebe 17 wa awali siku ya tukio walikamatwa eneo la Kawe wilaya ya Kinondoni.


Alisema watuhumiwa wengine 12 walikamatwa katika stendi ya mabasi ya Temeke wakiwasumbua abiria kupanda magari.
Watuhumiwa wote walikana shtaka na kesi yao imepangwa kutajwa Julai 16 na 17, mwaka huu.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents