Siasa

Wapinzani kuishtaki Serikali

VYAMA vya CUF, Chadema, NCCRMageuzi na TLP, vimepanga kufungua kesi
mahakamani pamoja na mambo mengine, kupinga wanafunzi wa Elimu ya Juu
kupewa mkopo wa asilimia 60 tu, hali iliyosababisha mgomo kwa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na matawi yake pamoja na SUA.

Shadrack Sagati

VYAMA vya CUF, Chadema, NCCRMageuzi na TLP, vimepanga kufungua kesi mahakamani pamoja na mambo mengine, kupinga wanafunzi wa Elimu ya Juu kupewa mkopo wa asilimia 60 tu, hali iliyosababisha mgomo kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na matawi yake pamoja na SUA.

Vyama hivyo kwa pamoja vimepanga kuwashitaki Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla kwa madai ya kuilazimisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuwakopesha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu asilimia 60 kinyume cha sheria.

Sheria inayodaiwa kuvunjwa (kwa mujibu wa vyama hivyo) na Prof. Msolla ni Sheria namba 9 ya mwaka 2004 ya Bodi hiyo ambayo inaeleza wazi kuwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao hawana uwezo kifedha watakopeshwa na Bodi hiyo asilimia 100.

Hata hivyo, HabariLeo imegundua kuwa Sheria hiyo inasema itasaidia kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye mahitaji ya lazima, hali ambayo inaweza kuwa ni kwa asilimia 100 au vinginevyo kwa jinsi Bodi ya Mikopo itakavyompima mwombaji. Vyama hivyo vimetangaza kufungua kesi kuiomba Mahakama iamuru wanafunzi kurudishwa chuoni bila masharti yoyote na walipwe fidia ya usumbufu wa kufukuzwa kwa kuwapa taarifa katika kipindi kifupi.

Licha ya kufungua kesi hiyo, vyama hivyo pia vimeanza mchakato wa kuwahamasisha wananchi kuandamana kushinikiza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na SUA kuwarudisha wanafunzi bila masharti yoyote.

Maandamano hayo kwa kuanzia yatafanyika mkoani Morogoro Mei 5, kutokana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kusimamishwa masomo. Baadaye maandamano hayo yatafanyika katika Jiji la Dar es Salaam siku itakayotangazwa na vyama hivyo. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni uongozi wa bodi ya mikopo ya elimu ya juu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Vyama hivyo vitafungua kesi hiyo wiki ijayo baada ya siku 21 walizozitoa kwa Serikali kumalizika. Vyama vitakavyofungua kesi hiyo ni Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Labour Party (TLP) na NCCRMageuzi.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Bodi ya mikopo na makamu mkuu wa chuo wamelazimishwa na Prof. Msolla kuvunja sheria hiyo ambayo haijawahi kufanyiwa marekebisho yoyote na Bunge.

“Waziri kama alikuwa na nia ya kubadilisha sheria hii angerudi bungeni, lakini ametufanya Watanzania mbumbumbu wa sheria hadi anakiuka sheria hii ambayo sasa inawatesa watoto wetu,” alisema Dk. Slaa. Katika mkutano huo ambao mzungumzaji mkuu alikuwa Profesa Ibrahim Lipumba, ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia pamoja na Katibu Mkuu wa TLP, John Komba.

Licha ya ukiukwaji wa sheria hiyo, sababu nyingine iliyotajwa na wapinzani hao ni kuweka msingi ya ubaguzi katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Ubaguzi huo ni kuwapa wanafunzi wa kiume mkopo wanaopata daraja la kwanza tu pamoja na wasichana wanaopata daraja la kwanza na la pili.

Sababu yingine inayoelezwa na wapinzani ni ukiukwaji wa haki ya kuishi na haki ya usalama waliyofanyiwa wanafunzi. Wanasiasa hao wanasema kitendo cha kuwapa saa tatu wanafunzi
kuondoka katika maeneo ya chuo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Naye Mbatia alisema wanafungua kesi hiyo baada ya tamko la chuo kikuu la juzi la kuwashinikiza wanafunzi watekeleze masharti yote kabla ya kurejea chuoni Mei 14. Tangazo hilo lilitolewa na Profesa Rwekaza Mukandala.

Alisema wanafunzi wengi wanaosoma chuoni hapo wazazi wao wana kipato kidogo hivyo kulipa asilimia 40 itakuwa mzigo kwao. Alisema Serikali iwakopeshe asilimia 100 kwa vile ni fedha ambazo zinarejeshwa. Profesa Lipumba akizungumza kwenye mkutano huo, alisema matamshi ya Rais Jakaya Kikwete kuwa hakuna mtoto wa maskini atakayefukuzwa chuo kwa kukosa ada hayatekelezeki na yamekiukwa.

Na John Nditi,anaripoti kutoka Morogoro kuwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) cha Morogoro umetoa masharti ya vipengele 11 vinavyowataka wanafunzi wa shahada ya mwaka kwanza na wa pili waliofanya mgomo wa kuingia madarasani wa muda wa siku tatu na kufukuzwa wawe wamerudi chuoni hapo ifikapo Mei 5, mwaka huu.

Masharti ya vipengele hivyo ni pamoja na kuwataka wanafunzi hao kuandika barua kwanza ya kuomba msamaha na kukubaliana na sheria na kanuni za chuo hicho pamoja na kanuni za mitihani na barua zao kuzituma chuoni hapo kwa njia ya rejesta, EMS na DHL na kumfikia Makamu wa Mkuu wa chuo kabla ya Mei 6, mwaka huu.

Masharti mengine barua zao za kuomba msamaha zionyeshe pia kiasi cha gharama halisi za mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Pia wametakiwa kuonyesha stakabadhi ya Benki itakayoonyesha kwamba malipo ya asilimia 40 na malipo ya gharama nyingine za chuo pia zimelipwa kabla hawajarudi chuoni hapo.

Wanafunzi hao wa shahada ya kwanza wa mwaka wa kwanza na wa pili walifanya mgomo chuoni hapo kuanzia Aprili 16 hadi 18, mwaka huu bila kuingia madarasani wakidai Serikali kuwalipia asilimia 100 ya mikopo badala ya asilimia 60 . Wanafunzi hao mbali na kutakiwa kulipia asilimia 40 na wao kutaka iondolewe pia walidai kuongezewa posho ya chakula na ile ya vitendo wakiwa nje ya chuo

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents