Habari

Wapinzani waing`ang`ania BoT

Kambi ya upinzani imesema inatarajia kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu Benki Kuu (BoT).

Na Joseph Shayo, Dodoma



Kambi ya upinzani imesema inatarajia kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu Benki Kuu (BoT).


Maelezo hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti bungeni na Kiongozi wa Upinzani, Bw. Hamad Rashid Mohamed (CUF Wawi), ambaye pia ni msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Fedha.


Mbunge mwingine aliyezungumzia suala la kuwasilisha hoja binafsi bungeni ni Dk. Wilbroad Slaa (Karatu CHADEMA) ambaye ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na msemaji wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.


Wakati tunakwenda mitamboni, taarifa za Bunge zilionyesha kuwa hoja hiyo binafsi itakayowasilishwa na Dk. Slaa, imepangwa kusikilizwa kati ya Agosti 10 hadi 17.


Akichangia wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha vifungu vya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge mwishoni mwa wiki, Bw. Hamad alisema: `Tutawasilisha hoja binafsi ya kutoridhika na uamuzi wa serikali kumteua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kushirikiana na kampuni ya ukaguzi kutoka nje ya nchi kufanya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu katika BoT.`


Wakati huo Bunge lilipokaa kama kamati, lilikuwa chini ya uenyekiti wa Spika, Samuel Sitta.


`Hilo la BoT, tutasubiri wakati muafaka,` alisema Spika Sitta akimtaka Bw. Hamad azungumzie mambo mengine na siyo suala la BoT.


Kwa mujibu wa Bw. Hamad, kambi ya upinzani inataka uchunguzi huo ufanywe na kamati teule ya Bunge na taarifa yake iwasilishwe moja kwa moja bungeni badala ya kuipeleke serikalini.


Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alielezea nia ya kuwasilisha hoja binafsi bungeni pale aliposimama wakati Bunge lilipoketi kama kamati ya matumizi chini ya uenyekiti wa Naibu Spika, Anna Makinda kupitisha vifungu vya makadirio ya bajeti ya matumizi kwa Wizara ya Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Dk. Slaa aliposimamishwa kuzungumza, alisema
hatozungumzia suala la BoT, isipokuwa suala hilo litazungumzwa wakati watakapowasilisha hoja binafsi.


Akizungumza wakati akifanya majumuisho ya mjadala wa bajeti ya Ofisi yake na Ofisi ya Bunge Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu Edward Lowassa alisema, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali atasimamia uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha ndani ya Benki Kuu na akakataa uchunguzi huo kufanywa na kamati teule ya Bunge.


Alisema hakuna haja ya kuunda kamati teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa tuhuma hizi, kwa kuwa serikali ina vyombo vyinavyoweza kufanya kazi hii kwa kushirikiana na wakaguzi wa nje na akawaomba wabunge kuwa na subira wakati suala hilo linashughulikiwa kwa taratibu na hatua zinazochukuliwa na serikali.


Alisema baada ya uchunguzi huo kukamilika, ripoti hiyo itawasilishwa bungeni na aliwaomba wabunge wavute subira wakati suala hilo linashughulikiwa.


Lakini kambi ya upinzani imekuwa ikidai kuwa kuna habari ambazo zimetolewa na watu wenye kuitakia mema Tanzania kupitia mtandao wa kompyuta (internet) kwamba dola za Marekani takriban milioni 800 zimeliwa ama kupotea kwa uzembe katika Benki Kuu.


Mbali na BoT kutumia fedha nyingi kuliko inavyostahili, inadaiwa kuwa katika ujenzi wa majengo ya minara miwili ya BoT (Twin towers), ujenzi ambao uliruhusiwa kuendelea licha ya baadhi ya wajumbe katika Baraza la Mawaziri kupinga, kiasi cha Dola za Marekani milioni 30.8, sawa na sh. bilioni 40 kinatuhumiwa kufunjwa katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje.


Upinzani umekuwa ukisema hauamini kama CAG atafanya kazi hiyo kama inavyotakiwa na bila matokeo yake kuingiliwa na serikali.


Kiongozi wa upinzani Bungeni, Hamad Rashid, aliwahi kusema bungeni kwamba kila mwaka CAG amekuwa akifanya ukaguzi BoT lakini miaka yote hajawahi kuja na ripoti inayoonyesha ubadhirifu.


Upinzani unasema, hata hivyo kwamba, kinachotakiwa kuchunguzwa na serikali ni sehemu ndogo tu ya jambo kubwa ambalo limekuwa likiitafuna nchi.


`External Auditor (Mkaguzi wa Nje) mtakayemleta atafanya ukaguzi kuzingatia external debts (akaunti za madeni ya nje). Sisi tunasema takriban dola milioni 800 zimepotea BoT,` alisema Hamad Rashid bungeni na kuongeza kwamba Katiba ya nchi inatoa haki kwa bunge kuchunguza jambo kubwa kama hilo.


Suala la ubadhirifu ndani ya BOT limekuwa moja ya ajenda kubwa tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti mwezi uliopita.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents