Habari

Wapinzani wajuta

‘MAJUTO ni mjukuu’; ndivyo inavyoonekana kuwa kwa upande wa vyama vitatu vya upinzani, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na Tanzania Labour (TLP)

na Kulwa Karedia na Asha Bani

 

‘MAJUTO ni mjukuu’; ndivyo inavyoonekana kuwa kwa upande wa vyama vitatu vya upinzani, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na Tanzania Labour (TLP), ambavyo ushirikiano wao uliolenga kukishinda Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa ubunge Tunduru, uligonga mwamba.

 
Hali hiyo ya kujutia kile kinachoonekena kuwa mbinu chafu za CCM, ilidhihirika jana wakati viongozi wakuu watatu wa vyama hivyo walipoitisha mkutano wa waandishi wa habari kuelezea yale yaliyowasibu Tunduru.

 
Kauli za viongozi hao watatu, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Augistine Mrema (TLP), zilikuwa ni marudio ya malalamiko yale yale ambayo wamekuwa wakiyatoa kila mara unapomalizika uchaguzi ama mkuu, wa marudio au mdogo, kama ule wa Jumapili iliyopita wa Tunduru.

 
Huku wakionekana dhahiri kusahau makosa ambayo wamekuwa wakiyafanya kila mara ya kuingia katika chaguzi chini wa mwamvuli wa sheria na taratibu zilezile, viongozi hao watatu walikitupia lawama nyingi chama tawala na vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi.

 
Kama walivyopata kusema wakati jeshi hilo likiongozwa na Omar Mahita, ambaye sasa amestaafu, viongozi hao wakuu walielekeza shutuma zao kwa Mkuu wa sasa wa jeshi hilo, IGP Said Mwema.

 
Katika kuonyesha namna walivyokuwa wameguswa na kushindwa kwao katika uchaguzi huo ambao mgombea wa CCM, Abdallah Mtutura, alitangazwa mshindi, viongozi hao kwa mara nyingine tena, walionya kuhusu kutoweka kwa amani hapa nchini iwapo vyama vyao vitaendelea kuminywa na kuhujumiwa wakati wa uchaguzi.

 
Viongozi hao walibainisha wazi kutokuwa na imani tena na IGP Mwema, kutokana na namna jeshi lake lilivyotumika katika uchaguzi huo kuvikandamiza vyama vya upinzani kwa manufaa ya CCM.

 
Walisema kuwa ushindi wa CCM huko Tunduru umepatikana kwa hila na iwapo hali hiyo itaendelea, taifa linaweza kuwa katika hali mbaya katika kipindi kifupi kijacho kwa sababu uvumilivu wao sasa umefika kikomo.

 
“Hatima ya Tanzania sasa inaelekea pabaya sana, amani imekuwa ikichezewa kila siku, na kibaya zaidi wanadhani wanatudhalilisha mimi na Lipumba… kumbe sivyo.

 
“Nilikuwa na imani kubwa sana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, lakini sasa naye ameonyesha kuvaa viatu vya mwenzake aliyepita, Inspekta Jenerali mstaafu Omari Mahita, aliyekuwa na tabia hii ya kupiga watu ovyo,” alisema Mrema.

 
Alisema halitakuwa jambo la ajabu siku wananchi watakapochoka na kuamua kuasi kwa kujichukulia sheria mkononi, ili kulipiza kisasi dhidi ya polisi wanaoshiriki kuwanyima uhuru wa kuchagua kiongozi wanayemtaka.

 
Mwanasiasa huyo ambaye kabla ya kwenda TLP alikuwa NCCR na kina Mbatia, kabla ya kukorofishana nao, alisema kitendo cha CCM kumsafirisha Mzee Rashid Kawawa hadi Tunduru, ni ufujaji wa fedha za umma.

 
Kwa upande wake, Mbatia alionya kuwa matendo ya vyombo vya dola yanatishia kuvunjika kwa amani na iwapo hilo litatokea, litasababisha matatizo makubwa nchini.

 
“Taifa liko katika vuguvugu ambalo linachochewa na CCM… napenda kueleza kwamba yakitokea machafuko tutaumia sote, lakini watakaoumia zaidi ni viongozi walioko madarakani kwa kushindwa kutekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi,” alisema Mbatia.

 
Mbatia alisema CCM imeshindwa kumuenzi mwasisi wa chama hicho, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. aliyehubiri amani, umoja na mshikamano kwa Watanzania wote.

 
Alisema endapo amani iliyopo itasambaratika, CCM itapaswa kubeba mzigo wote wa lawama kutokana na ubabe dhidi ya vyama vya upinzani.

 
Alinukuu maneno ya Baba wa Taifa aliyoyasema wakati wa kudai uhuru kuwa, ‘kama wakoloni hawajatupa uhuru wetu tutashitaki kwa Mungu na kama Mungu hatasikia kilio chetu, itabidi tushitaki kwa shetani,’ na kusema hayo ndiyo mambo yatakayotokea kwa chama tawala iwapo hakitajirekebisha.

 
Kwa upande wake, Profesa Lipumba alisema endapo serikali haitafanya marekebisho ya Katiba na kuunda Tume huru ya Uchaguzi, vyama vya upinzani havitashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

 
“Bila kuwa na katiba yenye msingi wa demokrasia inayohahakikisha kuwa Tume ya Uchaguzi inakuwa huru, itakuwa vigumu kwa vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi wa mwaka 2010, na hili tunalichukulia kwa uzito wote,” alisema Lipumba.

 
Kuhusu uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tunduru, mwenyekiti huyo alisema chama chake hakiyatambui matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

 
“Sisi CUF tunasema kwamba matokeo ya Tunduru hatuyatambui kwa sababu kulikuwa na hujuma na wizi mkubwa wa kura na vitendo vya rushwa vilitawala,” alisema Lipumba.

 
Alisema katika uchaguzi huo, mawakala wa CUF hawakuruhusiwa kusindikiza masanduku ya kupigia kura yenye, matokeo ya kura katika vituo vyao.

 
“Mbali ya mawakala wetu kuzuiwa kulikuwa na maofisa Usalama wa Taifa kwenye vyumba vya kuhesabisa kura kinyume cha utaratibu,” alisema Lipumba.

 
Alisema bado wanaangalia mazungumzo ya amani kati yao na CCM, na wakibaini kuwa kuna kiinimacho kinachofanyika, hawatakuwa na imani tena na chama hicho.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents