Habari

Wasanii wa Reggae Tanzania mnapitwa na wakati,

Kwanini muziki wa raggae Tanzania haukui? Kwanini hizi nyimbo za reggae zinazotolewa na wasanii hawa wachache tulionao hazivutii kibiashara?

Ukianza kujiuliza kwanini muziki wa reggae Tanzania umegeuka kama mtoto mbilikimo anayekua kiduchu kabla ya kufika muda akadumaa kabisa, unaweza ukajiumiza akili bure kwasababu zoezi hilo litakupasua kichwa.

Hakuna msanii wa reggae tangu enzi za marehemu Justine Kalikawe na mkongwe Innocent Galinoma aliyevuma tena. Wapo wanajaribu lakini nyimbo zao zinaishia kuchezwa na radio mbili tatu za Tanzania basi imetoka! Na tena nyimbo zenyewe zinachezwa kwenye vipindi vya reggae tu.

Hii ni 2012, unadhani wimbo wenye ujumbe uliotakiwa kutolewa mwaka 1958 utawaingia akilini wapenzi wa muziki? Si jambo baya na ukweli kabisa roots reggae bado inapendwa na watu lakini watu hao si wananchi wa kawaida. Roots reggae inapendwa na watu wenye hisia za kirastafarai ama wale wanaoisikiliza kutokana na msukumo wa ‘majani’. Hilo liko wazi!

Lakini nyimbo hizo haziwezi kumvutia sistaduu, mtu mzima na wengine wasio na mapenzi ya reggae. Kwanini nyimbo kama ‘Paper Loving’ ya Chris Martin inapendwa na watu wengi tena hata wasio na mapenzi ya reggae! Well, ni kwasababu reggae ya sasa imebadilika. Ukitaka kufanya biashara kwa kuimba muziki huo lazima ukubaliane na ukweli huo.

Huu si muda wa nyimbo za ukombozi zilizokuwa zinaimbwa enzi za ukoloni. Leo dunia ina matatizo tofauti kabisa. Njaa, ufisadi, maradhi, vita na mambo mengi ambayo kuyazungumzia yanahitaji ‘ladha’ kwenye reggae na si muziki mkavu. Ujumbe tu katu hautoshi kuufanya wimbo uwe mzuri. Watu wanapenda muziki mtamu, mdundo unaovutia na sauti yenye mvuto.

Reggae imepitia hatua kadhaa mpaka leo hii. Kama muziki mwingine, aina hiyo ya muziki inabadilika na kukua pia. Leo hii kuna kizazi kipya cha reggae nchini Jamaica. Kizazi cha leo hakifanani na kizazi cha akina Bob Marley, Peter Tosh, Horace Andy, Black Uhuru ama The Abyssinians waliokuwa wamejikita kwenye roots reggae.

Pia kazazi chao kina utofauti kidogo na kile cha reggae ya mwanzoni kabisa(skinhead reggae), ambayo ilitamba enzi za movement za Rastafari na kuingia kwenye mainstream ya muziki wa Jamaica kuanzia 1968 hadi 1970. Wasanii waliokuwa maarufu kwenye aina hiyo ni kama John Holt, Toots & the Maytals, The Pioneers na Symarip.

Baada ya roots pakazaliwa aina nyingine nyingi za reggae kama Dub poetry, Rockers style, Dancehall, Lovers rock, Ragga, ama raggamuffin, Reggae fusion nk.

Leo hii muziki wa biashara nchini Jamaica na duniani kote umetawaliwa na Reggae Fusion.

Ni muziki wenye mchanganyiko wa reggae ama dancehall ukiwa na ladha za muziki mwingine na hivyo kuwa kama hip-hop reggae, R&B reggae, jazz reggae, rock ‘n roll reggae, Indian reggae, Latin reggae, drum and bass reggae, punk reggae, polka reggae, n.k.

Aina hii ya reggae ilianza kujipatia umaarufu miaka ya 90 na leo hii ndo imepamba moto zaidi. Hapo ndipo pakaanzishwa mtindo wa Riddim. Yaani beat moja inatumiwa na wasanii wengi ambao kila mmoja anaimba kwa melody na ujumbe wake mwenyewe.

Wakati Jamaica imefikia hatua hiyo, sisi tuliouchukua utamaduni huo kutoka kwao tumebakia pale pale na wahasisi wakiwa kwenye hatua nyingine kabisa.

Ukisikiliza nyimbo za wasanii wa kizazi kipya cha reggae nchini Jamaica kama Gyptian, Morgan Heritage (hufanya roots pia), Big Signal, Alaine, Cecile, Ritchie Spice, Fanta Mojah, Chris Martin na wengine ni rahisi kuwapenda hata kama wewe si mpenzi wa reggae. Ni kwasababu muziki wao umechanganya ladha za muziki mwingine husasan R&B na hivyo kujikusanyia mashabiki wa R&B tu.

Kwanini wanamuziki wa reggae wa Tanzania wamebaki kufanya muziki ule ule wa enzi za ukoloni? Mbaya zaidi ni kama bado wanasikiliza nyimbo zile zile za akina Bob na kuzidharau hizi za sasa zenye wapenzi wengi zaidi na si marasta tu.

Kama wanafanya reggae kwa sababu ya hisia za roots basi watambue kuwa kamwe hawawezi kusonga mbele. Wataendelea kuwa na mashabiki wale wale wenye mizuka ya ‘Ganja’ wakati reggae ya leo inamshika kila mtu.

Tunaamini hakuna kinachoshindikana. Mbona Kenya wanafanya vizuri. Chukulia mfano nyimbo za Wyre, Uprising na Guarantee aliyofanya na ndugu wa kundi la Morgan Heritage Peter na Gramps. Nyimbo hizi zimemfikisha mbali sana Wyre na sasa akitaka kwenda Jamaica kupiga show atapokelewa kwa mikono miwili.

Wasanii wa reggae Tanzania amkeni sasa na muendane na mabadiliko ya muziki mnaofanya. Acheni kuishi maisha ya enzi za ukoloni. Hii ni 2012 muziki umebadilika.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents