Habari

Wasiolipa mikopo chuo kikuu sasa kufungwa

Kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Sh milioni saba ni adhabu inayopendekezwa katika muswada wa marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya mwaka 2004 uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana.

Shadrack Sagati, Dodoma

 

Watakaoshindwa kurejesha mikopo ya masomo katika vyuo vikuu sasa wataweza kufungwa, imefahamika.

 

Kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Sh milioni saba ni adhabu inayopendekezwa katika muswada wa marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya mwaka 2004 uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana.

 

Katika muswada huo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu sasa itakuwa na uwezo wa kuwapeleka mahakamani watu wote ambao wamefaidika na mkopo, lakini kwa makusudi wakashindwa kulipa.
Katika marekebisho hayo, inapendekezwa pia kuwa mwajiri atakuwa na wajibu wa kutoa taarifa zinazowahusu wafanyakazi walionufaika na mikopo ili kuepuka kushtakiwa.

 

Pia kuna hatua ambazo zitachukuliwa kuwadhibiti waajiri na wanafunzi walionufaika na mikopo, lakini wakashindwa kutoa taarifa ya namna ya kulipa mkopo huo.

 

Hatua hizo ni mtu yeyote ambaye amemwajiri aliyefaidika na mkopo wa bodi hiyo, halafu akashindwa kutoa taarifa kwa bodi ili kutoa utaratibu wa kufanya malipo, mtu wa namna hiyo atakuwa amefanya kosa la jinai na anaweza kutozwa faini ya Sh milioni saba au kwenda jela mwaka mmoja.

 

Na kama mwajiri, ni shirika au kampuni, mtendaji mkuu au mtu yeyote ambaye ni ofisa maduhuli wa shirika husika, ndiye atakayehusika na adhabu hiyo.

 

Na kwa makusudi ya kifungu hicho ili kiweze kutekelezeka, sheria ya makampuni inayowalinda watendaji wake kushtakiwa binafsi, haitahusika katika suala hilo la mikopo, muswada unaeleza.

 

Katika muswada huo, pia inapendekezwa kuwa mwajiri ambaye ameajiri mtu aliyesomeshwa kwa fedha za bodi hiyo na akashindwa kutoa taarifa kwa bodi kama sheria inavyomtaka, bodi itakuwa na mamlaka ya kudai shirika hilo kulipa kiasi chote anachodaiwa mkopeshwaji aliyeajiriwa.

 

Pia inapendekezwa kuwa mtu ambaye atakuwa kikwazo atakayemzuia ofisa wa bodi au wakala wa bodi hiyo ambaye atakuwa ameteuliwa kufanya kazi kwa niaba ya bodi asitekeleze majukumu yake chini ya sheria hiyo mpya, atakuwa ametenda kosa la jinai na atapelekwa mahakamani na akipatikana na hatia, atalipa faini ya Sh milioni saba au kwenda jela si chini ya mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

 

Maofisa wa bodi au mawakala wake watakuwa na mamlaka ya kufanya ukaguzi rekodi zozote kwa taasisi, makampuni, mashirika yanayoajiri kupata taarifa ya watu waliosomeshwa kwa fedha za bodi hiyo.
Katika sheria hiyo, pia bodi itakuwa na uwezo wa kufungua mashitaka mahakamani ndani ya miaka 10 tangu mhusika achukue mkopo kwa bodi hiyo.

 

Kiasi ambacho mkopaji atatakiwa kulipa baada ya kupata ajira kitapendekezwa na bodi hiyo kutokana na kipato chake, lakini pia kuna kifungu kinachopendekeza kuwa malipo hayo yasizidi theluthi moja ya pato halisi (net) ya mkopaji.

 

Katika sheria hiyo mpya, bodi ndiyo itakayokuwa inapendekeza kiasi au asilimia ambayo itamkopesha mkopaji na kiasi ambacho mkopaji, mlezi au mzazi atachangia kutokana na ada ya taasisi husika.
Kwa sasa, bodi hiyo inatoa asilimia 60 ya mkopo na mzazi au mlezi analazimika kuchangia asilimia 40.

 

Kiasi hicho kimelalamikiwa na wanafunzi, wazazi na wanasiasa kuwa ni ukiukwaji wa sheria hiyo.

 

Wakati fulani vyama vya siasa vya upinzani vilikuwa na mpango wa kufungua kesi mahakamani kupinga utaratibu huo wa serikali kuwa unapingana na sheria husika.

 

Lakini pia sheria hiyo itaipa mamlaka bodi hiyo, kufuta mkopo na kutaka mkopaji kurejesha fedha ambazo atakuwa amekopeshwa awali katika mkupuo mmoja, itakapobainika kuwa alitoa taarifa za uongo wakati wa kuomba mkopo husika ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashitaka.

 

Bodi itafanya hivyo chini ya amri ya 35 ya sheria ya mwenendo wa kesi za madai kwa urejeshaji wa mikopo.

 

Pia inapendekezwa kuwa mwajiri atakuwa na wajibu wa kutoa taarifa zinazowahusu wafanyakazi walionufaika na mikopo kuepuka kushtakiwa Licha ya muswada huo, serikali pia iliwasilisha muswada mpya wa sheria ya utalii wa mwaka 2007 na muswada wa sheria ya kurekebisha sheria ya utumishi wa umma mwaka 2007 ambayo yote ilisomwa jana kwa mara ya kwanza.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents