Siasa

Wasiwasi wa muafaka wazidi kutanda Zanzibar

TAMKO lililotolewa mapema wiki hii na Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu kukwama kwa mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa visiwani hapa, limeanza kuwachanganya wananchi kadhaa.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


TAMKO lililotolewa mapema wiki hii na Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu kukwama kwa mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa visiwani hapa, limeanza kuwachanganya wananchi kadhaa. Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa waliopo hapa, wameielezea hali hiyo ya kukatisha tamaa kuwa inaweza kuisababishia Zanzibar matatizo katika siku zijazo.


Wasiwasi huo unakuja siku chache tu baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kukutana na waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki hii na kuiomba jumuiya ya kimataifa kuingilia katika hali hiyo.


Lipumba ambaye katika mkutano wake huo na wanahabari alikuwa ameongozana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema, juhudi za chama chake kuyanusuru mazungumzo kati yao na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaonekana kukwama.


Akizungumzia hali hiyo, Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib, alisema kwamba busara zinahitajika baina ya pande zote mbili zinazohusika na mazungumzo hayo, CUF na CCM ili kuhakikisha kuwa muafaka unapatikana.


Hata hivyo, alisema kwamba, viongozi wa CUF lazima waendelee kuwa na subira kwa vile wananchi wengi bado wana imani kuwa Rais Jakaya Kikwete atatimiza ahadi yake ya kulitafutia ufumbuzi tatizo la mpasuko wa kisiasa Zanzibar.


Alionya kuwa mazungumzo hayo yakivunjika, gharama yake itakuwa kubwa, kwa vile umoja na mshikamano unaojitokeza sasa utavurugika.


“Viongozi lazima wawe na subira kwa kuweka mbele umoja wa kitaifa, kama mazungumzo yatavunjika hali ya kisiasa itatetereka,” alisema kiongozi huyo.


Khatib alisema kwamba wakati umefika kwa vyama vya CCM na CUF kukaribisha vyama vingine katika mazungumzo hayo, kwani penye wengi haliharibiki neno.


Alisema kwamba ni jambo la kushangaza baraza la ushauri la vyama vya siasa la taifa liliundwa na rais mstaafu, Benjamin Mkapa, lakini hadi sasa halijakutana kujadili hali ya kisiasa kutokana na Mwenyekiti wa chombo hicho, Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, kushindwa kuitisha vikao.


Alisema kwamba hatua ya kuanzishwa kwa baraza hilo ilichukuliwa baada ya tume ya rais ya kusimamia muafaka kumaliza muda wake.


Alisema kwamba kwa sasa hakuna haja ya taasisi za kimataifa kuingilia kati mazungumzo ya CCM na CUF bali vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu vishirikishwe katika mazungumzo hayo kwa manufaa ya taifa.


Khatib alisema kwamba kwa vile hivi sasa viongozi wa pande mbili wamekuwa wakishutumiana, hatua ya kuwemo kwa viongozi wengine kutoka katika vyama vingine, itaharakisha upatikanaji wa muafaka.


Naye Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Hamisi Ambali aliunga mkono ushauri huo na kubainisha kuwa, upo umuhimu wa vyama vyote vya upinzani kushirikishwa katika mazungumzo hayo ili kuona nani, kati ya CUF na CCM, anayepiga chenga kufikia muafaka wa kudumu.


Alisema kwamba iwapo mazungumzo hayo yatavunjika watakaoathirika ni Wazanzibari, hivyo ni muhimu viongozi wa CCM na CUF wakaweka mbele maslahi ya taifa badala ya kukumbusha makovu ya kisiasa.


“Mazungumzo yaendelee, lakini kusiingizwe mchezo mchafu wa kisiasa na pia nia ya dhati ionekane katika mazungumzo hayo,” alisema Ambari.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa UPDP, Haji Othman, yeye kwa upande wake, alisema kwamba, mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha demokrasia na utawala bora kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010.


Alisema kwamba kama kuna upande hauna nia njema na mazungumzo hayo, utakuwa unajidanganya kwa vile athari zake zitamgusa kila mwananchi, bila ya kujali ana itikadi ya chama au kundi gani.


“Mazungumzo haya yakivunjika yanaweza kuathiri hali ya utulivu iliyoanza kuonekana na kuna umuhimu mkubwa ya kuyanusuru,” alisisitiza.


Tangu kutolewa tamko la CUF na Profesa Lipumba, vijana wengi wakiwemo wafuasi wa chama hicho, wamekuwa wakikaa katika vikundi wakijadiliana na wakikitaka chama hicho kijiondoe kwenye mazungumzo na ajenda irejeshwe rasmi kwa wananchi.


Baadhi ya vijana wamesema kuwa walionyesha tangu mwanzo kutokuwa na imani na CCM kwa vile hayo ni mazungumzo ya mara ya tatu, ambayo mara zote yamekuwa yakikwama.


Wakizungumza katika eneo la Mkunazini na Mlandege, vijana hao walisema wanaamini Rais Kikwete ana nia njema ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar, lakini kikwazo kiko kwa wahafidhina katika CCM upande wa Zanzibar, ambao wanahofia maslahi yao binafsi.


Walisema kwamba wahafidhina hao wanaamini iwapo kutaundwa serikali ya mseto, itakuwa ndiyo mwisho wa vitendo vya ufisadi, ikiwemo matumizi mabaya ya mali za umma, uporaji wa ardhi na majengo ya serikali kwa shughuli binafsi.


“Mseto ndio unaosababisha kushindwa kwa mazungumzo haya, vigogo wa Zanzibar wanaamini kuwemo kwa wapinzani katika serikali ni sawa na tochi itakayomulika katika giza,” alisema Abdulahim Masoud, mkazi wa Michezani.


Katika chaguzi zote chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, vyama vya CCM na CUF vimekuwa vikipishana kwa idadi ndogo ya kura, hali ambayo husababisha malumbano makubwa, na baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema kwamba serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo suluhisho la migogoro Zanzibar.


Katika uchaguzi uliopita mgombea wa CCM, Rais Amani Abeid Karume alitangazwa mshindi kwa kupata kura 239,832, sawa na asilimia 53.2, wakati mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alipata kura 207,773, sawa na asilimia 46.1.


Matokeo hayo yalionyesha CUF ilishinda viti vyote 18 vya ubunge na uwakilishi Pemba na kupata kiti kimoja katika Jimbo la Mji Mkongwe Unguja, ambapo CCM ilipata viti 31 Unguja.


Hata hivyo, chama cha CUF baada ya kutangazwa matokeo hayo, kimetangaza msimamo wa kutoitambua Serikali ya Zanzibar, kwa madai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.


Tamko hilo la CUF kuhusu kusuasua kwa mazungumzo limekuja wakati tayari baadhi ya wafuasi wa CUF wakiwa wameshashona sare zenye rangi ya bluu na nyeupe, kujiandaa kushangilia kutangazwa kwa serikali ya mseto, Agosti 15.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents