Wateja wa M-PESA sasa kutuma pesa nchini Kenya

Kampuni kubwa za mawasiliano Afrika mashariki Vodacom Tanzania na Safaricom ya Kenya leo zimezindua huduma mpya ambapo kuanzia sasa zaidi ya wateja Milioni 7 wa M-Pesa waVodacom Tanzania wanaweza kutuma na kupokea pesa kwa watumiaji zaidi ya milioni 18 wa Safaricom M-Pesa ya Kenya.

001.MEZA LAUNCH
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa kutuma na kupokea pesa nchini Kenya kwa njia ya M-PESA. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam

Huduma hii mpya ambayo imebuniwa na makampuni haya yanayoongoza kutoka huduma za mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki itawawezesha wateja wake kutuma pesa kwa kutozwa viwango sawa na vinavyotumika katika nchi husika.

Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hii,Mkurugenzi
Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza alisema kuwa takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 2013 zaidi ya shilingi bilioni 200 zilitumwa kutoka Tanzania kwenda Kenya halikadhalika zaidi ya bilioni 1 zilitumwa kutoka Kenya kuja Tanzania.

“Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa fedha karibu shilingi bilioni 200 zilizotumwa nchi Kenya kutoka Tanzania zilitumwa kwa njia rasmi za utumaji fedha na inakadiriwa kuwa kiasi cha fedha hizo zaidi ya mara mbili zimetumwa kwa njia zisizo rasmi za utumaji fedha ikiwemo kutumia madereva na makondakta wa mabasi au kutumia ndugu na marafiki wanaosafiri,” amesema Meza.

“Tumeona ugumu wanaokabiliana nao wateja wetu kutuma fedha katika nchi jirani ya Kenya na tumepata suluhisho kwa kuleta huduma hii ambayo ni ya haraka na uhakika. Kuanzia leo hakuna sababu ya kutuma pesa kwa kumtumia dereva au kondakta wa basi au kutozwa gharama kubwa kutoka taasisi za kifedha unapolipa karo za watoto wanaosoma nchini humo,unaweza sasa kufanya malipo na kulipa ankkra mbalimbali kutoka pochi ya M-Pesa ukiwa umetulia nyumbani kwako,” amesema Meza.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Safaricom Bob Collymore alisema “Tunaamini tumefungua ukurasa mpya wa kuendeleza huduma ya M-Pesa kwa kuwezesha wateja wa Kenya na Tanzania kutumia huduma hii katika kutumiana fedha na kufanya malipo katika nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya,” alisema.

Alisema katika awamu hii ya kwanza iliyozinduliwa leo inawawezesha wateja kutuma pesa Kenya kama ambavyo wamekuwa wakituma hapa nchini, tofauti itakuwa wakati wa kutuma pesa kwenye simu kutakuwepo na kipengele kinachoonyesha kuwa wanataka kutuma pesa kwa M-Pesa ya Kenya na kuandika namba za mpokeaji kwa kutumia namba za Kenya yaani +254 na katika awamu ya pili ya huduma hii wateja wa Safaricom ya Kenya wataweza kutuma pesa kwa wateja wa Vodacom Tanzania kupitia huduma hii.”

Huduma ya M-Pesa inatolewa na makampuni ya Vodacom Tanzania na Safaricom ya Kenya yote yakiwa makampuni makubwa yanayotoa huduma ya mawasiliano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.Wakati Vodacom inatoa huduma za kutuma na kupokea fedha kwa asilimia 65 nchini.

“Ushirikiano huu wa mtandao wetu wa M-Pesa wenye mawakala zaidi ya 75,000 nchini Tanzania utawarahishia wateja wetu kupata huduma bora ikiwemo kufanya mihamala yao ya fedha kwa urahisi na tumejipanga kutoa huduma bora kwa wateja kwa muda wote wa masaa 24 kila siku,” alisisitiza Meza.

“Kenya ni moja ya nchi inayofanya biashara kwa kiasi kikubwa na Tanzania ndio maana huduma hii imeanzia nchini humo na kuzidi kuunganisha na kuimarisha ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.Tunaamini kuwa mawasiliano hayana mipaka kwa kuwa kwa kuwa huwaunganisha watu na jamii na jamii na kusaidia kuharakisha maendeleo na ndio maana Vodacom imekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika sekta hii,” alisisitiza Meza.

Kuna zaidi ya Wakenya 300,000 wanaotuma fedha nchini kwao kwa kutumia njia zisizo rasmi na salama kama vile kuwatumia makondakta na madereva wa mabasi vilevile kuna watanzania wengi wanasomesha watoto wao nchini Kenya ambao nao wamekuwa wakipata shida kutuma fedha nchini humo. “Kwa kuanzia leo huduma kwa wafanyabiashara kulipana zimerahisihwa ikiwemo kulipa karo za shule na vyuo na mihamala mingine,Huduma ya M-Pesa imerahisisha kila kitu na kuzidi kufungua milango ya biashara na ushirikiano, ” aliongeza kusema Meza.

Alimalizia kusema kuwa huduma hii itafanya maisha ya watumiaji wake kuwa murua kwa kuwa watatuma fedha zao na kuwa na uhakika wa kuwafikia walengwa moja kwa moja na ni njia ya uhakika na yenye usalama inayowapunguza adhabu kubeba kiasi kikubwa cha fedha mifukoni na kwenye mabegi pia walengwa watapokea malipo kwa viwango vya ubadilishanaji sahihi visivyobadilika kila siku.

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW