Habari

Watoto wa kike watakiwa kuwa chachu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia

Watoto wa kike nchini wameaswa kujitambua, kujiamini na kujilinda dhidi ya vishawishi vinavyosababisha matukio maovu ya Ukatili wa Kijinsia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni na kusababisha kukatisha ndoto zao za kupata haki ya kuendelezwa na elimu bora kwa manufaa yao, familia na Taifa.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt Faustine Ndugulile Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wakati wa uzinduzi wa klabu za wasichana katika shule ya Sekondari ya Mwendakulima.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinazidi kushamiri katika jamii zetu hususan katika meneo ambayo bado wanafuata mila na desturi ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike na mwanamke.

Ameongeza kuwa namna bora ya kupambana na ukatili wa kijinsia ni kwa watoto wa kike kutonyamaza pale ambapo wanafanyiwa vitendo vya ukatili hasa kuozeshwa na kushawishiwa kuingia kwenye mahusiano ya kingono katika umri mdogo: mambo yanayosababisha mimba na ndoa za utotoni.

“Kila mtu aunge mkono juhudi zetu za pamoja za kutokomeza mimba na ndoa za utotoni kwa kuacha usiri na kushirikiana kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa mamlaka zilizopo,“ alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulu amesema kuwa Wilaya yake inaendelea kushirikiana na jamii na wadau wa maendeleo katika kuendeleza juhudi za Serikali za Kupambana na Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni ili kuwapatia watoto wa kike haki yao ya kuendelezwa na kuwaandaa kuwa nguvu kazi bora ya Taifa la uchumi wa kati na wa viwanda.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents